Habari za Punde

Ajali mbaya yafungua mwaka. Saba wafa, 47 wajeruhiwa



Na Pascal Buyaga,Mara
WATU saba wamefariki papo hapo na wengine zaidi ya 47 kujeruhiwa vibaya baada ya mabasi mawili ya abiria kugongana uso kwa uso.
Miongoni mwa waliofariki ni wanawake wanne na wanaume watatu

Ajali hiyo mbaya kuwahi kutokea katika mwaka huu, ilitokea katika kijiji cha Nyatwari, tarafa ya Serengetu wilayani Bunda mkoani Mara.
Ajali hiyo iliyahusisha mabasi ya kampuni ya Mwanza Coach aina ya scania marcopolo lenye namba za usajili T756AWT mali ya   Halfan Ahmed ambalo lilikuwa likitokea Musoma kuelekea Mwanza na basi la kampuni ya Bestline  lililokuwa likitokea Mwanza kuelekea Sirari wilayani Tarime.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa polisi wa mkoa wa Mara, Absalom Mwakyoma alisema kuwa ajali hiyo ilitokea  majira ya saa 11 jioni katika eneo ambalo barabara kuu inafanyiwa matengenezo, hivyo kuwepo vumbi jingi kiasi cha madereva kushindwa kuonana.


Mwakyoma alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa mabasi hayo na madereva kutokuwa makini.
Majeruhi wamekimbizwa katika hospitali ya wilaya Bunda kwa matibabu.

Aidha alisema majeruhi 14 ambao hali zao ni mbaya wamepelekwa katika hospitali ya rufaa ya Bugando kwa matibabu zaidi.

Baadhi ya abiria walikuwemo kwenye mabasi hayo walisema mabasi hayo yalikuwa yakiendeshwa kwa mwendo wa kasi na licha ya kuwataka madereva wapunguze mwendo lakini hawakusikilizwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.