Habari za Punde

Cannavaro, wenziwe waitwa Taifa Stars


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
 
WACHEZAJI watatu waliofungiwa kucheza soka mwaka mzima na Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), ni miongoni mwa walioitwa na kocha mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen, kwa ajili ya mechi za kirafiki.
 
Juzi, Poulsen alitaja wanasoka 22 ambao wanatakiwa kuanza kambi Januari Januari 6, mwaka huu mjini Dar es Salaam kwa ajili ya mechi hizo ambazo ni sehemu ya maandalizi ya mechi ya mashindano dhidi ya Morocco iliyopangwa kuchezwa mwezi Machi mwaka huu.


Wachezaji ambao ZFA imetangaza kuwafungia na kulitaka Shirikisho la Soka Tanzania kutowatumia kwenye timu ya taifa, ni Nadir Haroub ‘Cannavaro’ anayechezea Yanga, Aggrey Morris na Khamis Mcha, wote wa Azam FC. Hata hivyo, beki wa Simba Nassor Masoud, hakuitwa kutokana na kukabiliwa na majeraha.
 
Poulsen amewataka wachezaji hao kuripoti kambini katika hoteli ya Tansoma mnamo saa 11.30 jioni ya siku hiyo, tayari kwa mazoezi yatakayoanza Januari 7, mwaka huu.
 
Wachezaji walioitwa ni walinda mlango Juma Kaseja (Simba) ambaye ndiye nahodha wa Stars, Aishi Manula na Mwadini Ally (wote Azam), pamoja na mabeki Aggrey Morris na Erasto Nyoni (Azam), Amir Maftah (Simba), Issa Rashid (Mtibwa Sugar), Kelvin Yondani na Nadir Haroub (Yanga) na Shomari Kapombe (Simba).
 
Viungo ni Salum Abubakar na Khamis Mcha (Azam), Athuman Idd na Frank Domayo (Yanga), Amri Kiemba na Mwinyi Kazimoto (Simba), pamoja na Shabani Nditi (Mtibwa Sugar).
 
Washambuliaji ni John Bocco (Azam), Mbwana Samata (TP Mazembe-DRC), Mrisho Ngasa (Simba), Simon Msuva (Yanga), na Thomas Ulimwengu wa TP Mazembe, (DRC).

4 comments:

  1. Mukiambiwa Zanzibar si nchi hamuamini, haya oneni sasa, mpaka ZFA wabara hawaitambui!

    Nyinyi mumewafungia wachezaji, lakini ni kama kutwanga maji kwenye kinu, hao wanaendelea kupeta Bara washaitwa Taifa, kwa wenye nchi!

    Kazi kwenu kama mutaendelea na mfumo uliopo au mutashikamana muachiwe mupumuwe!

    ReplyDelete
  2. Tuache siasa 'issue' hapa sio kua Z'bar ni nchi au laa bali inaonekana ni kutokuelewana kimaamuzi kati ya ZFA na wenzao wa TFF!

    ReplyDelete
  3. Haya maamuzi hayana mantiki utamfungia mchezaji kwa kugawana dola elfu kumi kila mchezaji dola mia tano, badala ya kuwapongeza na kuwatafutia pesa nyengine kwa ari na ushujaa wao na jinsi ya kuonesha kiwango kizuri. ZFA ni viongozi wachoyo sana. TFF mmefanya jambo la maana sana

    ReplyDelete
  4. Bado Zanzibar politics need mainland collaboration. Bado misuguano ya kihistoria haijakwisha na hakuna dalili ya kwisha kwa hii generation. Hata hao wanaoshabikia utengano hawatakuwa salama endapo utengano unaoishi kwa miongo mingi bado ipo.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.