Na Mwandishi wetu
WAKATI mitambo ya analogi ikizimwa rasmi usiku wa saa sita wa Januari 1, 2013, asilimia 95 ya wananchi wa Zanzibar wamejikuta wakiamka bila ya kuwa na matangazo ya televisheni.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, umebaini nyumba nyingi zikiwa hazina matangazo ya televisheni, isipokuwa kwa wale wanaotumia ving’amuzi ambao bado ni wachache mno.
Maeneo yote ya vijijini huduma za matangazo ya televisheni yamekatika kabisa isipokuwa matangazo yanayorushwa na Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC), ambalo hata hivyo bado halijaingia katika mfumo huo.
Wananchi wa Zanzibar walikuwa wakitegemea kupata matangazo ya televisheni kutoka vituo mbali mbali vya televisheni Tanzania Bara, ambavyo vilikuwa na mitambo ya kurusha matangazo jijini Dar es Salaam.
Kwa sasa hawapati tena matangazo yanayorushwa na vituo vyote vya televisheni vya Tanzania Bara.
Jiji la Dar es Salaam ndio la kwanza kuingia katika mfumo mpya wa mawasiliano wa dijitali.
Hali hiyo sasa inawafanya wananchi kuwa na chaguo moja tu la kupata matangazo ya televisheni kupitia ZBC isipokuwa kwa wale wenye ving’amuzi.
Bado ni gharama kubwa kupata ving’amuzi kwa wananchi wa Zanzibar kutokana na gharama zake ikilinganishwa na pato la wananchi wake, ingawa huduma hiyo ipo.
Akizungumza na waandishi wa habari wiki iliyopita, Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar, Said Ali Mbarouk alisema Zanzibar itaingia katika mfumo wa dijitali mwezi Februari.
Shughuli za uwekezaji mitambo katika kituo kikuu cha dijitali kilichopo Rahaleo mjini Zanzibar bado unaendelea.
Wakizungumza na gazeti hili, wananchi walieza kushangazwa kwao kukosa matangazo ya televisheni, wakisema kamwe hawakutarajia.
Walisema hawakufikiria kwamwe kwamba kuzimwa mitambo ya analogi jijini Dar es Salaam kungesababisha athari katika maeneo mengine ikiwemo Zanzibar.
“Sisi tulitarajia tungeendelea kufaidika na matangazo ya televisheni kama kawaida lakini kwa kweli tumeshangazwa,” walisema.
Mmoja ya wananchi hao mkaazi wa Mwanakwerekwe aliliambia gazeti hili kwamba, watoto wake walimuagiza awanunulie karata ili wapate kucheza hasa ikizingatiwa kwamba katika kipindi hichi skuli zote za umma zimefungwa.
Gazeti hili ambalo lilitembelea nyumba nyingi , liliwakuta watoto, kike kwa kiume na watu wazima wakiangalia michezo ya kuigiza ya kiswahili kupitia DVD zao.
Hali hiyo sasa inawafanya kukosa taarifa muhimu kama taarifa za habari na matangazo mengine yanayorushwa kupitia television
No comments:
Post a Comment