Habari za Punde

Kichanga kilichotupwa charejeshwa kwa mama yake


Na Masanja Mabula,Pemba
 
UONGOZI wa Shehia ya Tumbe Mashariki kwa kushirikiana na jeshi la polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba pamoja na maofisa wengine kutoka ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Micheweni umefanikisha kumrejesha kwa mama yake mtoto mchanga ambaye alitupwa muda mfupi baada ya kuzaliwa.

Kichanga hicho chenye umri wa karibu siku 10 sasa kiliokotwa na wasamaria wema muda mfupi baada ya kutupwa na mama yake kikiwa na umri wa chini ya saa moja.

Kabla ya kuunganishwa na mama yake, kichanga hicho kilikuwa kinalelewa na mkunga wa jadi Aminia Fadhil Sahaaban.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Sheha wa Shehia ya Tumbe Mashariki, Seif Omar alisema uongozi wa shehia ulipokea taarifa ya kuokotwa kichanga hicho Disemba 19 mwaka jana na akachukua hatua za kuwasiliana na vyombo vinavyohusika.

Alisema kichanga hicho kilokotwa na Mariam Issa Nassor na Said Omar Ali kikiwa bado hakijafanyiwa usafi na kisha kukipeleka kwa mkunga wa jadi ambaye alikisafisha na kuendelea kukitunza.

"Raia wema walikiokota kichanga hicho na kisha kukipeleka kwa mkunga wa jadi , Bi Aminia ambaye yeye alikisafisha na kisha kuendelea kukipa huduma zote mpaka kufikia leo (jana ) tulipofanikiwa kumtambua mama yake na kumkabidhi,” alisema Sheha huyo.

Sheha huyo alisema uongozi wa shehia utamtembelea mama wa mtoto huyo aliyetajwa kwa jina la Kioni Said Juma (30) pamoja na kufuatilia maendeleo ya mtoto huyo ambaye hali yake inaendelea vyema.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na mwandishi waa habari hizi walisema kuwa iko haja kwa serikali kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria dhidi ya mwanamke huyo ambaye alikuwa na lengo la kukatisha uhai wa mtoto asiyekua na hatia.

Juhudi za mwandishi wa habari hizi kukutana na mama wa mtoto huyo kuzungumzia sababu ya kumtupa mtoto huyo ziligonga mwamba baada ya wazazi wake kukataa katu katu kufanya mazungumzo na vyombo vya habari.

Bado sababu za mtoto huyo kutupwa hazijajulikana, lakini watu wa karibu walisema ni kutokana na kutelekezwa na mwanamme aliempa ujauzito, kwa sababu mwanamke huyo bado alikuwa hajaolewa.



1 comment:

  1. Katika nchi zilizoendelea na zenye ustaarabu na ambazo zinzendeshwa kwa hatua za haki na kisheria, mtoto huyo hawezi kupelekwa kwa mama yake katu.

    Mama huyo ni mfalifu na hana uwezo wa kumlea mtoto huyo kwa sababu kama aliweza kumtupa akiwa hai kwa nini asiweze kumdhuru baadae na hata kumuua?

    Huyo ni muhalifu na muhalifu mahala pake ni jela maisha. Kumrejesha mtoto huyo kwa mama huyo ni kudhihirisha namna gani nchi isivyozingatia haki na sheria na kutokuthamini maisha ya mtu.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.