Habari za Punde

‘Watakaouza mipira ya mradi kukiona’

Na Ameir Khalid
  HATUA kali za kisheria, zitachukuliwa dhidi ya mtu yeyote atakaebainika kuuza mipira ya msaada itayotolewa na serikali bila ya malipo kwa klabu mbalimbali za soka hapa Zanzibar.
 
Onyo hilo limetolewa jana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk mbele ya waandishi wa habari na watendaji kadhaa wa sekta ya michezo kwenye ukumbi wa VIP uwanja wa Amaan.
 
  Alisema kwa kuwa mipira hiyo itatolewa bure, serikali haitamvumilia mtu yeyote atakaepatikana akifanya mradi wa kujiingizia fedha kwa maslahi binafsi kutokana na mipira hiyo.


Alifahamisha kuwa, mipira ipatayo elfu ishirini inatarajiwa kutolewa na Serikali ya Zanzibar kupitia wizara yake, kwa klabu zote za Zanzibar ambapo uzinduzi wake umepangwa kufanyika Januari 10, mwaka huu ukiongozwa na Rais Dk. Ali Mohammed Shein atakaekuwa mgeni rasmi.
 
Waziri huyo alisema jumla ya klabu elfu moja, mia moja na ishirini Unguja na Pemba, zitanufaika na mradi huo, ambapo mipira hiyo itagawiwa kwa timu za ligi kuu, vijana, skuli, mpira wa mikono na netiboli, ikifaidisha vijana laki tatu kwa kila klabu ya kupata mipira mitatu.
 
Alisema mradi huo ni miongoni mwa jitihada za serikali kuendeleza sekta ya michezo kwa kushirikiana na wahisani na miradi mbalimbali, ikiwemo kutoa mafunzo kwa makocha na ujenzi wa viwanja vya michezo katika kila wilaya.
 
  Mpira hiyo imetolewa jina la kampuni ya Chevrolet, na itasambazwa na Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ), likishirikana na Shirikka la Kuhudumia Watoto la Kimataifa (Save the children), na mashirika mengine yanayojishughulisha na masuala yanayohusu ukatili dhidi ya watoto Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.