Na Mwandishi wetu
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dk. Mohammed Gharib Bilal ameiwakilisha Tanzania katika
mazishi ya mpigania uhuru na mwanaukombozi wa Afrika, Komredi Landa John Nkomo
yaliyofanyika katika makaburi ya mashujaa wa Zimbabwe, mjini Harare.
Komredi Nkomo hadi anafikwa na
mauti alikuwa Makamu wa Rais wa Zimbabwe na Makamu Mwenyekiti wa chama cha ZANU-PF
kinachoongozwa na Rais Robert Mugabe.
Nkomo alifariki Januari 17, 2013
nchini Afrika Kusini alikopelekwa kwa matibabu baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa
kansa kwa miaka kadhaa na alifariki akiwa na umri wa miaka 79.
Mazishi hayo yaliongozwa na Rais
Mugabe na yalihudhuriwa na Makamu wa
Rais wa Afrika Kusini, Zambia, Botswana na Namibia.
Maelfu ya wananchi wa Zimbabwe
walihudhuria mazishi hayo huku wakionekana kuguswa na msiba huo mkubwa, hali
iliyowafanya kutokuondoka katika eneo la mazishi hata pale mvua ilipokuwa
ikinyesha.
Rais Mugabe wakati akilihutubia
taifa alisema, hayati Nkomo alikuwa mfano thabiti wa amani katika Afrika na
hata wakati anapelekwa Afrika Kusini kutibiwa alikuwa kinara katika mazungumzo
ya kufikia mkataba wa makubaliano ya vyama vya siasa juu ya katiba
itakayotumika kwa jili ya uchaguzi mkuu ujao nchini Zimbabwe, makubaliano
yaliyopitishwa mapema juma lililopita.
Akizungumza na Dk. Bilal Ikulu
jijini Harare, Rais Mugabe aliishukuru Tanzania kwa kuwa mshirika na ndugu wa
karibu katika hali zote za maisha ya wananchi wa Zimbabwe na akafafanua kuwa
udugu katika nchi hizo ni wa kutukuka na unatakiwa kulindwa na kuenziwa kwa
vizazi vingi vijavyo.
Katika ziara hiyo fupi, Dk. Bilal licha
ya kuhudhuria mazishi ya Nkomo, pia alipata fursa ya kumtembelea Rais Mugabe
ofisini kwake ikulu jijini Harare na kisha kukutana na baadhi ya Watanzania
waishio Zimbabwe katika makazi ya balozi wa Tanzania.
Katika maelezo mafupi aliyoyatoa
kwa wananchi wa Tanzania waishio Zimbabwe, Dk. Bilal aliwataka kujiuliza kuhusu
mambo yapi wanaona ni muhimu na bora kwa kuutangaza Utanzania na Mtanzania na
kuwataka kuyatumia hayo hasa sasa wakati nchi inapoendelea na mchakato wa
mabadiliko ya katiba ili yawe chachu ya uzalendo na taswira kwa kila Mtanzania
kama yalivyo mataifa mengine.
Watanzania hao pia waliitaka
serikali ya awamu ya nne kuwaelimisha wananchi wa Mtwara kuhusu umuhimu wa gesi
kutumika kwa maendeleo ya taifa na wakamuomba Dk. Bilal kuwaelimisha wananchi
hao.
No comments:
Post a Comment