Na Mwantaga Ame
TATIZO
la kukatika mara kwa mara kwa umeme limesababisha kikao cha Baraza la
Wawakilishi kushindwa kufanyika jana asubuhi.
Hali
hiyo ilijitokeza wakati kikao hicho kikiendelea katika kipindi chake cha
masuala na majibu.
Kabla
ya Spika wa Baraza hilo Pandu Ameir Kificho, kuamua kuahirisha kikao hicho
umeme huo ulikatika ghafla baada ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Baraza la
Mapinduzi, Mwinyihaji Makame kumaliza kujibu suala la Mwakilishi wa jimbo la
Chaani, Ussi Jecha Simai.
Kutokana
na hali hiyo Spika Kificho, alitoa tangazo la kuahirisha kwa muda kikao hicho
na kuwataka wajumbe wa Baraza hilo
kusubiri hadi umeme huo urudi.
Hata
hivyo, wakati Spika akijitayarisha kutoka katika ukumbi huo huduma ya umeme
ilirudi na kuwataka wajumbe hao kuendelea na kikao hicho.
Wajumbe
hao walianza kikao hicho lakini pia walijikuta wakiifanya kazi hiyo kwa muda
mfupi baada ya umeme kukatika tena jambo
ambalo lilimfanya Spika kutoa tangazo la moja kwa moja kuwataka wajumbe kutoka
katika kikao hicho.
Akiahirisha
kikao hicho Spika huyo, alisema asingeweza kuendelea na kikao hicho kwa sababu umeme
uliokuwa ukiwaka usingeweza kumudu kuendesha na vipoza hewa kutokana na kiwango
chake kuwa kidogo.
Alisema
hali hiyo ingeliweza kusababisha hali ya afya za baadhi ya wajumbe kuathirika.
Spika
alisema kutokana na hali hiyo imemlazimu kuahirisha kikao hicho kwa vile tayari
Shirika la Umeme lilishalitaarifu baraza hilo
kuwa limo katika matengenezo baada ya kutokea hitilafu katika baadhi ya mitaa
ya eneo hilo.
Alisema
kwa vile hakuna uhakika wa muda gani wa mafundi wa shirika hilo wataweza
kufanikiwa kukamilisha urejeshaji wa huduma hiyo,kikao hicho hakitaweza
kuendelea hadi wakati wa jioni.
Kuahirishwa
kikao hicho kulisababisha masuala yapatayo tisa kutoulizwa yakiwemo yanayohusu
umeme, chumba cha wagonjwa mahatuti ,ICU, elimu ya juu, shirika la bandari,
ushajiishaji wananchi katika kilimo cha umwagiliaji maji, uvunjaji wa
shirika la magari na utengzaji wa
barabara.
Tatizo
la kukatika umeme lilikuwa kubwa juzi usiku katika maeneo mengi ya Zanzibar.
Wakaazi
wa eneo la Kisimamajongoo, Kikwajuni, Michenzani, Mazizini na Chukwani walikosa
huduma hiyo kwa siku ya pili jana baada
ya kukatika nyakati za saa 2:15 usiku ambapo hadi jana mchana huduma hiyo ilikuwa
haijarudi.
Hata
hivyo wananchi wa Kikwajuni na Kisimamajongoo wameilalamikia hali hiyo kwa
kujitokeza mara kwa mara ya kukatika umeme kunakosababishwa na kuunguwa kwa
Trasfoma iliopo eneo la Kisimamajongoo.
Wananchi
hao walieleza huenda ikawa tatizo hilo
linatokana na trasfoma iliyowekwa ikawa ni ndogo kulingana na uwezo wa watumiaji
kwani imekuwa ikiripuka mara kwa mara.
Ni
siku chache tu wakati yakitokea ahayo Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Iddi
alikaa na viongozi wa Shirika la Umeme na kuwataka kuona awanatekeleza majukumu
yao vyema
kutokana ana kuongezeka kwa vitendo vya ukatikaji wa huduma ya umeme mara kwa
mara.
Hata
hivyo sababu kubwa ambayo Shirika la Umeme imekuwa ikiitoa juu ya kuwepo kwa
suala hilo ni
kutokana na kuwepo kwa mabadiliko ya utandazaji wa waya mpya wa huduma ya umeme
chini ya mradi wa MCC.
Hapo
awali Shirika hilo
lilitangaza kuwa litakamilisha kazi hiyo mwezi Disemba mwaka jana lakini tayari
wametoa tarehe nyengine ya kukamilisha kazi hiyo kufikia mwezi Februari hadi
Machi mwaka huu.
No comments:
Post a Comment