Habari za Punde

Balozi Seif ataka uadilifu wasimamizi wa TASAF


Na Othman Khamis, OMPR
MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF), Ladislaus Mwamanga amesema mradi wa Tasaf awamu ya tatu unatarajiwa kulenga zaidi katika miradi ya elimu, afya na maji safi ili kusaidia zaidi kupunguza umaskini kwa wananchi wanaoishi katika mazingira magumu.

Hatua hiyo itakwenda sambamba na uimarishaji wa uongozi katika mifumo ya utekelezaji wa miradi hiyo ambayo ni muhimu kwa maslahi ya wananchi walio wengi.

Mwamanga aliyaeleza hayo wakati alipouongoza ujumbe wa viongozi watano wa Tasaf kutoka makao makuu Dar es Salaam kuzungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ,Balozi Seif Ali Iddi ofisini kwake Vuga.

Alieleza kwamba Tasaf awamu ya tatu imekusudia kupanua wigo kwa kuendelea kuzishirikisha Halmashauri za Wilaya kwa upande wa Tanzania Bara wakati Zanzibar zitaendelea na hatua ya awali kwa shehia 20 kwa kuzijengea mifumo ya utekelezaji.


Alisema Zanzibar imefanikiwa vyema katika utekelezaji wa Tasaf awamu mbili zilizopita na kuiomba ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais ambayo ndio inayoratibu shughuli za Tasaf Zanzibar kumteua ofisa atakayekuwa na majukumu ya kuratibu shughuli zote za Tasaf kwa upande wa Zanzibar.

Akitoa shukrani zake, Balozi Seif alisisitiza suala la kuongezwa taaluma kwa watendaji wanaosimamia miradi hiyo.

Alisema kumekuwa na ubadhirifu na matumizi mabovu yaliyokuwa yakifanywa na baadhi ya wasimamizi wa miradi katika awamu zilizopita tabia ambayo imezorotesha kutokukamilika au kufa kabisa kwa baadhi ya miradi.

Aliwaasa watendaji wote wanaopewa jukumu la kusimamia miradi ya Tasaf kujitahidi kuzingatia uadilifu ili kuepuka ujanja unaobuniwa na baadhi ya wahujumu wa miradi hiyo kwa maslahi binafsi.

Aliupongeza Uongozi wa Tasaf kwa uamuzi wake wa kuzingatia zaidi kutoa taaluma kwa watendaji watakaopewa jukumu la kusimamia miradi ya Tasaf.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.