Habari za Punde

Mashirika yatakiwa kuwatumia wakaguzi wa serikali



Na Mwantanga Ame
SERIKALI imetakiwa kuacha kitumia wakaguzi binafsi katika kufanya ukaguzi wa mahesabu katika mashirika yake na badala yake watumie wakaguzi wa serikali walio chini ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG).

Mwakilishi wa Amani, Fatma Mbarouk aliyasema hayo wakati  akichangia mswada wa sheria wa kuanzisha shirika la meli Zanzibar, katika kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachoendelea mjini Zanzibar.

Mwakilishi huyo alisema serikali inapaswa kuliangalia suala hilo kutokana na  kuzoeleka kwa mashirika mengi yaliopo kuamua kufanya ukaguzi kwa kuyatumia makampuni binafsi jambo ambalo limekuwa likichangia uchelewaji wa kueleweka mahesabu ya serikali.

Alisema mashirika mengi yamekuwa yakifanya ukaguzi wake kuanzia  Januari hadi Disemba lakini serikali imekuwa ikifanya hivyo kati ya mwezi Julai jambo ambalo linaweza kuleta migongano ya kiutendaji.

Alisema kwa vile Mkaguzi wa serikali ametajwa ndani ya katiba ya Zanzibar , ni vyema akapewa hadhi ya kuyakagua mashirika badala ya kuendelea kutumia wakaguzi binafsi wakati serikali imekuwa ikiajiri na kuwasomesha wataalamu wa fani hiyo.


Alisema kuyatumia makampuni binafsi katika kufanya ukaguzi wa serikali kunaweza kukasababisha usumbufu kwa kamati za baraza la Wawakilishi.

Alisema kuja kwa mswada huo utawezesha kulifanya shirika la meli, kuwa mfano bora katika uendeshaji kwa kujipangia shughuli zake na kuachwa lijiendeshe wenyewe kwani mfumo wa sasa hauwezi kulifanya kuwa bora kutokana na kutegemea mkono wa serikali kujiendesha.

Aliseaama kazi kubwa inayotakiwa kufanywa ni viongozi wa wizara kutoa mamlaka kamili kwa shirika hilo.

Nae Mwakilishi wa Kiwani, Hijja Hassan Hijja akitoa maoni yake alisema ni lazima mashirika ya umma yawe na Idara za ukaguzi kwani baadhi ya mashirika yanakwepa hilo ili kuweza kufuja mali za serikali.

Aidha, Mwakilishi huyo aliiomba wizara husika  kuona uteuzi wa bodi ya shiriaka hilo unakuwa na wajumbe watakaolifanya shirika kuwa na tija.

Nae Mwakilishi wa Chonga, Abdalla Juma, akitoa maoni yake alisema ipo haja sheria hiyo inaweka muda maalum wa kumfanya Mkurugenzi kupeleka mahesabu yake kwa mkaguzi mkuu ndani ya kipindi cha mienzi mitatu badala ya kuacha kuwepo uhuru usiokuwa na kikomo.

Nae Mwakilishi wa Kitope, Makame Mshimba Mbarouk, akitoa maoni yake alisema ipo haja ya serikali kuotumia wataalamu wake kulifanya shirika la meli kuwa lenye mabadiliko kama inavyotokea katika mamlaka ya uwanja vya ndege Zanzibar.

Alisema mamlaka ya uwanja wa ndege hivi sasa imeonesha  mabadiliko makubwa kutokana na kuwepo uongozi wenye kuleta tija.

Mwakilishi wa Wawi, Nassor Saleh, aliipongeza serikali kuleta barazani mswada huo kwani utazuiya kulifanya shirika hilo kufanya kazi zake kiholela kamaa lilivyo sasa.

Naye Mwakilishi wa Micheweni, Shubeit Khamis Faki, akitoa mchango wake alisema mswada huo unahitaji kuliona shirika litakaloundwa linajiendesha kibiashara balada ya mtindo wa sasa wa kuwa na majina ya mashirika amabayo hayana tija kwa taifa.

Nae Mwakilishi wa viti vya wanawake, Mgeni Hassan, alisema ni vyema wizara ikazingatia ushauri wa kamati kuona wajumbe wa bodi wanaoteuliwa hawatoki katika serikali pekee.

 MapemaWaziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Rashid Hemed Seif, alisema kuja kwa mswada huo kutaweza kuimarisha kazi za shirika hilo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.