Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa
Balozi Seif Idd, Makamu wa Pili wa
Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar;
Waheshimiwa
Mawaziri;
Waheshimiwa
Mabalozi;
Wawakilishi
wa Mashirika ya Kimataifa;
Viongozi na watendaji wakuu wa Serikali;
Viongozi wa Vyama vya Siasa, Viongozi wa Dini, Viongozi wa
Jamii; Wanahabari;
Wageni
Waalikwa;
Mabibi na
Mabwana;
Nashukuru kwa
kunialika kuja kushiriki kwenye tukio hili muhimu na la kihistoria la kutangaza
matokeo ya awali ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012. Haya ni matokeo ya
kazi ya kuhesabu watu iliyofanyika kwa siku 14 kuanzia tarehe 26 Agosti, 2012
hadi 4 Septemba, 2012.
Ndugu wananchi;
Napenda
kutumia nafasi hii kutoa pongezi za dhati kwa wale wote waliofanikisha zoezi la
kuhesabu watu na wale waliokamilisha uchambuzi unaotuwezesha leo kutangaza
idadi ya Watanzania ilivyo sasa. Kwanza
kabisa napenda kutambua Kamati ya Taifa ya Sensa iliyoongozwa na Mheshimiwa
Mizengo Peter Kayanza Pinda, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa na Mheshimiwa Balozi Seif Ali Idi,
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akiwa Mwenyekiti upande wa Zanzibar. Nawashukuru kwa uongozi wao mzuri ambao
matunda yake ndiyo haya yanayotukusanya leo.
Pia nawashukuru wajumbe wa Kamati za Sensa za Mikoa na Wilaya nchini.
Pili, napenda kuwatambua viongozi na
wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya Jamhuri ya Muungano chini ya
uongozi wa Mama Albina Chuwa na wenzao wa Afisi ya Mtakwimu Mkuu wa Zanzibar
chini ya uongozi wa Ndugu Mohammed Hafidh Rajab. Nawapongeza kwa umahiri wao katika kuongoza,
kuratibu na kisimamia utekelezaji wa jukumu lenyewe la kuhesabu watu. Ni wao kuliko mtu mwingine ye yote ndiyo
waliokabidhiwa kazi ngumu ya kutengeneza mipango na taratibu za kufanya zoezi
lenyewe. Walitayarisha madodoso,
kuyachapisha, kuyasambaza, kuteua watu wa kuhesabu watu na wasimamizi wao. Waliwafundisha wajibu wao na kuwasimamia
katika utekelezaji wao. Ni wao pia waliohakikisha
kuwa madodoso yote yanakusanywa na uchambuzi unafanywa mpaka sasa tuko tayari
kutangaza matokeo.
Nawatambua
na kuwashukuru makarani wa sensa waliopita nyumba kwa nyumba kuhesabu watu na
kukusanya taarifa mbalimbali kwa mujibu wa madodoso waliyokuwa nayo. Tunatoa shukrani na pongezi maalum kwao kwa
sababu ni wao hasa waliowezesha kupatikana taarifa itakayotangazwa leo na
nyingine zitakazofuatia siku za usoni.
Kama si wao tusingekusanyika hapa
leo. Nawapongeza kwa umakini wao na moyo
wao wa uvumilivu na uzalendo. Haikuwa
kazi rahisi kwa ukubwa wa kazi yenyewe. Pia,
walikumbana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na baadhi ya maeneo kuwa na
mazingira magumu ya kufanyia kazi kama vile ya usafiri. Lakini pia kulikuwa na
ugumu wa kupata taarifa kutoka kwa wanaoulizwa. Baadhi hawakutoa ushirikiano
unaotakiwa. Yalikuwepo pia matatizo ya
kupata huduma stahiki za kufanyia kazi na hasa posho. Nafahamu kuwa wapo bado wanaodai stahili zao. Hazina wamekiri hilo na kuahidi watalimaliza
haraka.
Ndugu wananchi;
Kufanya sensa ni kazi
kubwa na ghali sana. Hata hivyo nchi
zote duniani hufanya sensa kwa sababu ya umuhimu wake. Kupitia Sensa, hupatikana taarifa muhimu za
kutumiwa na Serikali kupanga mipango ya maendeleo ya nchi na jinsi ya kuhudumia
wananchi. Taarifa hizo hutumika na wadau
mbalimbali katika shughuli zao za kuwahudumia wanadamu. Ndiyo maana madodoso yalikuwa na mambo mengi
na ndiyo maana tumeambiwa kuwa taarifa ya leo ni ya mwanzo tu. Zipo taarifa zitakazofuatia zenye uchambuzi
wa mambo mbalimbali. Naomba tuwe na subira kwa taarifa mbalimbali tunazozitaka, kwani tutazipata
wakati wake utakapofika. Kwa niaba yenu
niwaombe wahusika wafanye kila wawezalo kuhakikisha kuwa taarifa hizo
zinapatikana kwa wakati uliopangwa.
Ndugu Wananchi;
Nitakuwa mwizi wa
fadhila kama sitawatambua watu wengine wafuatao: Wa
kwanza ni Hajat Amina Mrisho, Kamishna wa Sensa ambaye tulimkabidhi jukumu
la kutoa uongozi wa kisiasa katika kazi ya kuhesabu watu na kuwa kiungo kati ya
wataalamu na uongozi wa Serikali. Vile
vile, tulimpa kazi ya kusaidia kufikisha ujumbe pande zote ili kuona kuwa mambo
yanakwenda vizuri. Bahati nzuri
mwenyewe ni mjuzi wa masuala ya takwimu.
Alitokea huko kabla ya kumchukua na kumleta katika shughuli za uongozi
wa kisiasa. Hivyo, kazi ilikuwa mikononi
kwa mwenyewe. Namshukuru kwa kuifanya
kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa. Anao
mchango mkubwa katika mafanikio haya. Wa pili ni wananchi wa Tanzania. Nawashukuru kwa ushirikiano wao. Kabla na wakati wa Sensa, kulikuwa na purukushani
na maneno mengi ya upotoshaji na kutishia kuvuruga zoezi lenyewe. Wapo wenzetu walioamua kuendesha kampeni ya
kutaka watu wasusie. Wapo walioamua
kufanya maandamano na mikutano ya siasa wakati huo na jitihada zote za kuwasihi
wasubiri siku 14 zipite walizipuuza.
Wakati mwingine unashindwa kuelewa baadhi yetu tuna dhamira gani katika kujihusisha
na shughuli za siasa? Hivi inakuwaje washindwe kutambua umuhimu wa kuhakikisha
jambo kubwa kama hili linafanikiwa? Hivi zoezi la sensa lisipofanikiwa kiongozi
wa siasa au wa dini unanufaika nini? Ndiyo
maana nawashukuru sana wananchi kwa ushirikiano wao uliofanya njama za kuvuruga
zoezi kushindwa.
Ndugu wananchi;
Wa
tatu ni Wajumbe wa Kamati za Sensa za
Mikoa na Wilaya kwa kufanikisha zoezi la Sensa katika Mikoa na Wilaya zao. Nawashukuru
Wakuu wa Mikoa na Wilaya wote nchini kwa uongozi wao mzuri. Wa nne
ni viongozi wa kijamii wakiwemo wa vyama
vya siasa, madhehebu ya dini na wa kimila waliosimama kidete kuhamasisha
wafuasi wao kushiriki katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi. Tunawashukuru
kwa mchango wao muhimu. Wa tano ni wamiliki wa vyombo vya
habari na wana habari. Nawashukuru kwa
kufanya kazi kubwa na nzuri ya kuhamasisha na kuelimisha jamii katika kipindi
chote cha utekelezaji wa zoezi la Sensa. Wito wangu kwenu ni kwamba, endeleeni
kuelimisha na kuhamasisha matumizi ya
taarifa za Sensa kwa maendeleo ya taifa letu.
Wa
mwisho, lakini siyo kwa umuhimu, nawashukuru
sana washirika wetu wa maendeleo wakiwemo UNFPA, DFID, JICA, CIDA na Benki ya
Dunia kwa mchango na msaada wao mkubwa. Nawashukuru Wenzetu hawa wametupa
ushirikiano mkubwa uliotuwezesha kufanikisha zoezi la Sensa hadi kufikia hatua hii
ya sasa ya kutoa matokeo ya awali. Naomba washirika wetu wa maendeleo waendelee
kushirikiana nasi kukamilisha kazi hii na pia katika kuimarisha sekta ya
takwimu nchini.
Ndugu wananchi;
Baada ya kusema maneno
hayo sasa nipo tayari kuzindua rasmi matokeo ya awali ya Sensa ya Watu na
Makazi ya mwaka 2012. Kwa heshima na
unyeyekevu mkubwa natangaza kuwa kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi
iliyofanyika kwa siku 14 kuanzia Agosti 26, 2012, Tanzania ina watu 44,929,002 ambapo Tanzania Bara kuna watu 43,625,434
na Zanzibar kuna watu 1,303,568. Katika Sensa ya tatu ya mwaka 2002
tulikuwa milioni 34.4 hivyo
tumeongezeka kwa watu milioni 10.5 ongezeko
ambalo ni sawa na asilimia 2.6 kwa
mwaka. Naomba taarifa hizi zitumike kwa
madhumuni yaliyokusudiwa ambayo ni kuboresha maisha ya kila Mtanzania.
Ndugu Zangu;
Hii ni Sensa ya nne
kufanyika nchini tangu kuasisiwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka
1964. Sensa ya kwanza ilifanyika mwaka
1967 ambapo nchi yetu ilikuwa na watu 12,313,054.
Tanzania Bara ilikuwa na watu 11,958,654 na Zanzibar watu 354,400. Kwa maana hiyo, katika miaka 45 tangu Sensa ya kwanza na hii,
Watanzania wameongezeka kwa watu milioni
33.
Ndugu Wananchi;
Kama kasi ya ongezeko
la watu la asilimia 2.6 halitapungua
ifikapo mwaka 2016 nchi yetu itakuwa na watu milioni 51.6. Inawezekana idadi hiyo ikaonekana kuwa siyo tatizo la kuumiza
kichwa kwa nchi kubwa kama yetu, lakini ni mzigo mkubwa kwa taifa, jamii na
uchumi kuwahudumia. Inabidi pawepo na
mikakati madhubuti na ionekane katika mipango ya maendeleo kuanzia sasa jinsi
ya kuhudumia watu hao 51.6 na zaidi
ya hao miaka inayofuata. Kwa familia,
lazima tutambue umuhimu wa kupanga uzazi, vinginevyo hali ya maisha itashuka
sana. Kwa ujumla hatuna budi kufanya
kazi kwa bidii zaidi na nguvu zaidi.
Asanteni sana kwa
kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment