Na Pascal Michael,Bunda
RAIA wa kigeni kutoka China, Mark Wang
Wei amekamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani
Bunda wakati akijaribu kumuhonga Mkuu wa Wilaya hiyo rushwa ya shilingi 500,000
ili kampuni yake ipewe zabuni ya kusambaza pembejeo za kilimo wilayani humo.
Wang ni Mkurugenzi wa kampuni ya
Panda International Co. Ltd.
Akizungumza na waandishi wa habari
ofisini kwake, Mkuu wa wilaya ya Bunda, Joshua Mirumbe alisema baada ya kushtukia
jaribio hilo
aliweka mtego uliofanikisha kukamatwa.
Alisema Mkurugenzi huyo alimtumia
ujumbe mfupi kwa njia ya simu (sms) akimwambia kuwa anamletea zawadi ya ahsante ofisi kwake jambo lililomshangaza Mkuu huyo
wa wilaya kwa kuwa alikuwa hajui kazi aliyofanya kiasi cha kupewa ahsante.
Mirumbe alisema Wang ni mmoja ya
mawakala wanaotumiwa kusambaza pembejeo za kilimo na alitakiwa kuwasilisha
kibali cha kuishi nchini na cha
kufanya kazi ili aingie mkataba na Halmashauri ya wilaya hiyo kwa ajili ya kusambaza pembejeo za kilimo
lakini baada ya kuoneka muda wake wa kuishi nchini unamalizika alinyimwa kibali
hicho.
Lakini alisema raia huyo alifika
ofisini kwake akiwa na barua kutoka Idara ya Uhamiaji ikimtambulisha kuwa
kibali chake cha kuishi nchini kimeongezwa hadi Machi.
"Nilishangaa, kwa kawaida
barua zote zinapaswa kupelekwa
masjala lakini raia huyu aliniletea moja kwa moja ofisini kwangu barua iliyotoka Idara ya Uhamiaji
ikimtambulisha kuwa anacho kibali cha
kuishi nchini hadi mwezi Machi na baadae
akanikabidhi bahasha ya fedha.
Nikamuuliza fedha hizo ni za nini akaniambia ni
ahsante, nikamuuliza ahsante ya
nini au kazi gani niliyofanya, akaanza
kubabaika ndipo nilipowaita TAKUKURU
ambao wapo karibu na kumkamata,” alisema.
Fedha hizo zilihesabiwa mbele ya
mashahidi na kuonekana ni shilingi 500,000.
Raia huyo atafikishwa mahakamani
baada ya uchunguzi kukamilika.
Akihojiwa na waandishi wa habari, Mchina
huyo alikiri kutoa fedha hizo huku akisitiza kuwa alimpa Mkuu huyo wa Wilaya kama
‘zawadi’ na kwamba hiyo siyo rushwa.
Kaimu Afisa kilimo wa wilaya ya
Bunda, Masuke Ogwa, aliwaambia waandishi wa habari kuwa kampuni ilikuwa bado haijaruhusiwa kusambaza pembejeo
wilayani humo, kutokana na kutokuwa na vielelezo vinavyotakiwa vya kumruhusu kuishi
nchini.
No comments:
Post a Comment