Habari za Punde

Wawakilishi: Sheria zinazotungwa zitekelezwe



Na Hafsa Golo
WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi wamesikitishwa na vitendo vya kutosimamiwa na kutotekelezwa sheria zinazopitishwa na baraza hilo.
Wawakilishi hao walieleza hayo  wakati wakichangia mswada wa sheria ya marekebisho ya sheria ya usafiri wa baharini nambari 5 ya mwaka 2006 katika kikao cha baraza la wawakilishi kinachoendelea mjini hapa.

Mwakilishi wa Jimbo la Kiwani, Hija Hassan Hija alisema Zanzibar kumekuwa na sheria nyingi lakini hazisimamiwi ipasavyo jambo ambalo limekuwa likisababisha kutokea kwa matatizo mengi.

Alisema mswada huo ni muhimu kwa maisha ya watu hivyo ni lazima sheria isimamiwe ipasavyo ili kuwaondolea majanga wananchi.

“Kila siku tumekuwa tukipitisha sheria lakini usimamiaji wa sheria ni mbaya na hivyo kuwapa mwanya watu kufanya wanavyotaka jambo ambalo linasababisha matatizo kwa watu wetu” alisema.

Aidha Hamza Hassan Juma (Kwamtipura), alisema Zanzibar ni nchi inayoongoza kwa kuwa na sheria nyingi lakini kutokana na usimamizi mbovu wa sheria hizo ndiko kunasababisha matatizo mbalimbali.

“Zanzibar inaongoza kwa kuwa na sheria nyingi Afrika lakini usimamiaji na utekelezaji wake ni mbaya na ndio maana kukawa na matatizo mbalimbali yanayotokea kila siku,” alisema.


Alisema sheria ya usafiri wa baharini ni muhimu kwa maisha ya wananchi na nchi kwa hivyo ni lazima kuwe na usimamizi madhubuti wa sheria hiyo.

Nae Mwakilishi wa jimbo la Muyuni, Jaku Hashim Ayoub, alisema usimamiaji wa sheria bado ni mbovu.
Kwa upande wake Mwakilishi wa nafasi za wanawake, Mgeni Hassan Juma,alisema bila ya kuwa makini katika utekelezaji wa sheria nchini,wananchi watakuwa wanaendelea kutumia huduma ya usafiri wa baharini kwa kubahatisha.

Aidha alisema wakati umefika hivi sasa kuondoa muhali katika usimamizi wa utekelezaji wa sheria hasa ikizingatiwa kumekuwa na sheria nyingi zilizopitishwa katika baraza ikiwemo unyanyasaji wa wanyama, lakini hazitekelezwi.

Nae Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed, alisema serikali itachukua jitihada kuhakikisha ajali zilizotokea za meli hazitokei tena na kama zitatokea ziwe za bahati mbaya sana.

Alisema majanga makubwa ya kuzama meli mbili muda mfupi yameiumiza serikali na wananchi kwa ujumla kwa kupoteza mali na roho za watu jambo ambalo linapaswa kuangaliwa kwa umakini mkubwa.
Aidha alisema kuwa Mamlaka za Usafiri Baharini za ZMA na SUMATRA ni lazima zihakikishe zinashirikiana kuhakikisha wanasafiri wanakuwa salama na mali zao.

 Mapema Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mawasiliano na Ujenzi ya Baraza la Wawakilishi, Hassan Hamad Omar, alisema sekta ya usafiri wa baharini ni lazima  ufanyiwe marekebisho kutokana na sekta hiyo kuchangia mapato ya nchi yanayotokana na uwekezaji.

Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Rashid Seif Suleiman alisema lengo la marekebisho ya  mswada huo, ni kuleta mabadiliko katika uendeshaji wa majukumu ya taasisi ya mamlaka ya usafiri wa baharini  na kuweza kufanyakazi zake kwa ufanisi zaidi na kuondosha changamoto ambazo zingeweza kuwakwaza kutokana na kutokidhi haja utumiaji wa sheria zilizopo.

Aidha  alisema marekebisho  hayo ambayo yatachunguza na kutilia mkazo zaidi juu ya usalama wa abiria na mabaharia katika vyombo vya baharini  na kuweka msisitizo juu ya matumizi ya vyombo vyenye ubora na viwango kilingana na sheria za kimataifa za (IMO).

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.