Habari za Punde

Baraza la biashara Zanzibar kesho



Na Kauthar Abdalla
MWENYEKITI wa Baraza la Biashara Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein ataongoza mkutano wa baraza hilo utakaojadili suala la ubia na uwekezaji katika sekta ya viwanda nchini.

Mkutano huo ambao utawakutanisha wataalamu wa masuala ya viwanda nchini na nje ya nchi utafanyika katika ukumbi wa salama hoteli ya Bwawani kesho.

Katibu Mtendaji Baraza hilo, Ali Vuai aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za baraza hilo Kinazini mjini Zanzibar.

Alisema mkutano huo utawakutanisha pamoja wadau kutoka sekta za umma na binafsi  kwa lengo la kujadili mambo muhimu ya maendeleo ya biashara kwa manufaa ya serikali na wajasiriamali.
Alisema suala la ubia na uwekezaji katika viwanda linaweza kuleta maendeleo makubwa  kwa Zanzibar.


Aidha alisema sekta ya viwanda iko nyuma sana hivyo mkutano huo utakuwa fursa muhimu wa kuandaa mikakati ya kuhakikisha viwanda vinafufuliwa na vyengine vipya vinaanzishwa.

Katibu huyo alisema nchi  haiwezi kuwa  na uchumi imara bila ya kuwa na viwanda bora ambavyo pia vitatengeneza fursa mpya za ajira nchini.

Alifahamisha kuwa  Baraza pia litatoa fursa kwa sekta binafsi kutoa kero zao ili Serikali ijue majukumu katika utendaji wa sekta hiyo pamoja na kutoa fursa kwa wajasiria mali kutangaza na kuuza bidhaa zao.

Hata hivyo alielezea kuwa wana lengo la kuangalia mwenendo mzima wa viwanda ili kujua Zanzibar ina mwelekeo gani wa kimaendeleo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.