Haji Nassor na Ali Khamis, Pemba
ZAIDI ya shilingi 227 milioni,
zimetumiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF), ili kufanikisha
miradi saba ya maendeleo kwa wananchi mbali mbali kisiwani Pemba, ikiwa ni
pamoja na mradi wa ujenzi wa barabara ya Matale- Chambani.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa
na Mratibu wa TASAF kisiwani humo, Issa Juma Ali, kati ya fedha hizo zaidi ya
shilingi 78 milioni zimetolewa na wananchi wenyewe katika kuunga nguvu miradi
hiyo.
Alisema shilingi 149 milioni
zilitolewa na TASAF awamu ya pili, kwa miradi hiyo ambapo baadhi
imeshakamilika.
Aliitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja
na ujenzi wa barabara ya Matale- Chambani yenye urefu wa kilomita 1.3 ambao
umegharimu zaidi ya shilingi 44 milioni ambapo fedha zote zilitolewa na TASAF
na wananchi kuchangia nguvu kazi.
Mradi mwengine ni upandaji miti
uliopo shehia ya Chumbageni wilaya ya Mkoani ambao umegharimu shilingi
35,995,850 ikiwa ni mchango wa TASAF pekee na wananchi pamoja na kikundi cha
ushirika kuchangia nguvu kazi.
Mratibu huyo wa TASAF aliutaja
mradi mwengine ambao pia wanajamii hawapaswi kuchangia ni ule wa kilimo cha
umwagiliaji maji uliopo shehia za Mgogoni na Wawi wilaya ya Chake Chake.
Katika awamu ya kwanza kwa shehia ya
Wawi, TASAF ilitoa zaidi ya shilingi 39 milioni, na awamu ya pili ya mradi huo
kwa shehia ya Mgogoni TASAF ilitoa zaidi ya shilingi 44 milioni.
“Miradi kama hii mara zote TASAF
haiwalazimishi wanajamii kuchangia na badala yake wao hupata ajira ya muda kwani
hushiriki katika kazi mbali mbali kama vile uchimbaji wa misingi na kuchota
udongo na kisha kulipwa,” alieleza Mratibu huyo wa TASAF.
Hata hivyo ameitaja miradi ya
ufugaji wa kuku wa mayai na ufugaji wa ng’ombe wa kienyeji na mbuzi kuwa
wanajamii hupaswa kuchangia fedha kwa asilimia 20 na kiasi kilichobakia
hutolewa na TASAF.
Alifafanua kuwa mradi wa ufugaji wa
kuku wa mayai uliopo shehia ya Mbuguwani wilaya ya Mkoani kuwa jumla ya
shilingi 10 milioni zilitumika kwa kufanikisha mradi huo.
Kati ya fedha hizo jamii yenyewe
ilichangia shilingi 490,000 wakati TASAF ilitoa zaidi ya shilingi 9 milioni
sawa na asilimia 80 ya gharama za mradi huo.
Kuhusu mradi wa ufugaji wa ng’ombe
wa kienyeji, kuku pamoja na mbuzi uliopo shehia ya Jombwe Mwembe wilaya ya Mkoani,
Mratibu huyo alisema, miradi hiyo imewanufaisha wananchi 108 wanaounda vikundi
9 wakiwemo wanawake na wanaume.
Alisema mradi wa ng’ombe pekee
umegharimu zaidi ya shilingi 58 ambapo umehusisha ununuzi wa ng’ombe 65 wakiwa
madume watano na kuhusisha vikundi vitano vya wananchi wa shehia hiyo.
Alifafanua kuwa kati ya fedha hizo
jamii ilichangia zaidi ya shilingi milioni 28 na TASAF ulitoa shilingi zaidi ya
shilingi 30 milioni.
Kuhusu miradi mitatu ya ufugaji wa
mbuzi wa asili na mmoja wa ufugaji wa kuku, alisema jumla ya shilingi milioni
87 zilitumika, ambapo TASAF ilitoa zaidi ya shilingi 44 milioni, na wanajamii
wenyewe walichangia shilingi 43 milion.
Mratibu huyo wa TASAF aliwataka
wananchi waliofaidika na miradi hiyo kuhakikisha wanaitunza na kuienzi ili iwe
endelevu na kuwanufaisha wao na kizazi kijacho.
Aidha alisema TASAF awamu ya tatu
iko njiani na itaangalia pamoja na miradi mikubwa ili kuzidi kuwang’arisha
wananchi kimaendeleo katika maeneo yao
siku hadi siku.
No comments:
Post a Comment