Na Husna Mohammed
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania
(TMA) kanda ya Zanzibar, inakusudia kufungua
ofisi yake bandarini Zanzibar kwa lengo la kuimarisha shughuli zake.
Ofisi za mamlaka hiyo inatarajiwa
kufunguliwa wakati wowote kuanzia mwezi wa Machi mwaka huu.
Akizungumza na gazeti hili ofisini
kwake, Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo Zanzibar, Khamis A. Suleiman, alisema
wameamua kufungua ofisi hiyo kwa lengo la kusogeza karibu huduma kwa wananchi
katika eneo hilo la bandari.
“Kwa kuwa sehemu zinazotumika kwa
usafiri kama viwanja vya ndege ni lazima kuweko na ofisi hivyo tumezingatia kwa
kina kufungua ofisi bandarini kwa ajili ya kuwapa taarifa wananchi kwa urahisi taarifa
za hali ya hewa,” alisema.
Hata hivyo, Mkurugenzi huyo alisema
wamekuwa wakikabiliwa na upungufu mkubwa wa vitendea kazi jambo ambalo linawapa
ugumu katika kutekeleza majukumu yao.
Alisema kiujumla mtandao wa vituo
vya kupokea taarifa bado ni mdogo Unguja na Pemba jambo ambalo linachangiwa na
upungufu wa vifaa.
Mamlaka ya hali ya hewa Zanzibar ni
moja ya taasisi muhimu ambayo imekuwa ikitoa taarifa za mara kwa mara za hali
ya hewa kwa wananchi na hasa wasafiri, wakulima na wanaotembelea mwambao wa
pwani ya Afrika Mashariki.
No comments:
Post a Comment