Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Prof. Palamagamba Kabudi akiongea katika mkutano na Chama cha United Democratic (UDP) wakati chama hicho kilipowasilisha maoni yake kuhusu Katiba Mpya katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam leo (Jumatatu, Jan 7, 2013).
Picha na Tume ya Katiba.
Na Mwandishi Wetu
Tume ya Mabadiliko ya Katiba leo (Jumatatu, Jan. 7, 2013) imeanza mikutano ya ndani ya kukusanya maoni ya makundi, vyama, asasi na taasisi mbalimbali kuhusu Katiba Mpya.
Mikutano hiyo inafanyika jijini Dar es Salaam katika Ofisi za Tume hiyo na ukumbi wa Karimjee.
Kwa siku ya leo (Jan. 7, 2013), Tume ilikutana na vyama saba (07) vya siasa ambavyo ni Chama cha Mapinduzi (CCM); Chama cha Wananchi (CUF); Chama cha NCCR-Mageuzi; Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Chama cha Tanzania labour (TLP); Chama cha United Democratic (UDP) na Chama cha Tanzania Democtratic Alliance (TADEA).
Katika mikutano hiyo, vyama hivyo viliwasilisha maoni ya vyama vyao kwa maandishi na kuzungumza na baadae wajumbe wa Tume walipata fursa ya kujadiliana na viongozi wa vyama hivyo kuhusu masuala mbalimbali.
Mikutano hiyo inatarajiwa kuendelea tena kesho (Jumanne, Jan 8, 2013). Mikutano hiyo ya Tume na makundi mbalimbali inatarajiwa kumalizika tarehe 25 Januari mwaka huu (2013). Baada ya mikutano hiyo, Tume itafanya uchambuzi na baadae kuandaa rasimu ya Katiba itakayochapishwa katika magazeti mbalimbali na baadae kuwasilishwa katika Mabaraza ya Katiba nchini kote mwezi Juni, mwaka huu (2013).
Mwisho.
No comments:
Post a Comment