KAMPUNI ya simu za mkononi ya Vodacom imetoa msaada vyakula na vitu vingine
kwa vituo vinne vya kusadia watumiaji wa dawa za kulevya kuachana na dawa hizo
(sober House) vilivyopo kisiwani Pemba.
Katika ziara hiyo ambayo ilimjumuisha Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa, kampuni hiyo mbali na kutoa msada wa vyakula
ilitoa dawa za kusafishia vyoo, sabuni.
Akizungumza mwishoni mwa wiki katika vituo kilichopo Chakechake, Profesa
Mbarawa, aliwataka vijana kuhakikisha matumaini waliyoyaonesha ya kutaka
kuachana na matumzi ya dawa hizo hayapotei.
Alisema uamuzi waliouchukua wa kutaka kuachana na matumizi ya dawa hizo ni wa
msingi na unawawezesha kurudi katika maisha yao ya kawaida sanjari na kutimiza
ndoto za maisha walizokuwa nazo.
“Nimejulishwa kwamba kuingia katika nyumba hii ni lazima mtumiaji mwenyewe
ukubali kuwa yupo tayari kuachana na dawa za kulevya. Hilo ni jambo jema na
linalonyesha mnayo matumaini ya kurudi katika maisha ya kawaida ,” alisema.
Aidha, alieleza kuwa serikali imekuwa ikifanya juhudi kukomesha biashara hiyo
na kwamba hata mawaziri wameshawahi kuoneshwa mikanda ya video inayoonesha
athari za dawa za kulevya.
Awali, Meneja wa Vodacom Foundation, Grace Lyon alisema kampuni hiyo imefika
katika nyumba hizo ikitekeleza kwa vitendo dira yake ya kusaidia makundi yenye
uhitiji kupitia programu ya ‘Pamoja na Vodacom’ inayotekelezwa kwa michango ya
wafanyakazi na kampuni.
“Tatizo la dawa za kulevya sio la mtu mmoja linatugusa sote kama sio ndani ya
familia basi kuna ndugu, jirani au hata rafik. Wito wangu mkubwa ni kuwaomba
kujitahidi kuhakikisha hamrudii kutumia dawa hizi,” alisema.
Kwa upande wake, Meneja Mahusiano ya Nje wa Vodacom, Salum Mwalim, alipongeza
utayari wa viijana hao kuachana na matumizi ya dawa hizo.
Chanzo - Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment