Hassan Hamad OMKR
Waislamu nchini wametakiwa kuyaendeleza matendo mema yaliyoasisiwa na maulama mbali mbali, ili kujenga jamii yenye maadili na kuendeleza taaluma zenye manufaa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Wito huo umetolewa na imamu wa Masjid Gof Mkunazini Zanzibar Sheikh Mudh-hirddin Ally Kullatein katika khitma maalum ya kumuombea marehemu Sheikh Said Mohammad Al-bir aliyefariki dunia hivi karibuni nchini Kenya akiwa na umri wa miaka 73.
Khitma hiyo hiyo pia ilihudhuriwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar al-hajj Maalim Seif Sharif Hamad pamoja na Mufti Mkuu wa Zanzibar sheikh Saleh Omar Kabi.
Akitoa wasifu wake baada ya khitma hiyo, sheikh Mudh-hirddin Kullatein amesema marehemu sheikh Said Mohammad Al-bir ametoa mchango mkubwa kwa Zanzibar katika kuendelea taaluma ya dini ya kiislam.
Amesema katika uhai wake aliweza kuasisi darsa zipatazo mia moja pamoja na misikiti kadhaa katika maeneo mbali mbali ya Afrika Mashariki ikiwemo Zanzibar, mambo ambayo yanapaswa kuendelezwa.
Nae ndugu wa karibu wa sheikh huyo sheikh Said Ahmed amesema msiba wa kuondoka kwa sheikh huyo sio wa watu wa Lamu pekee ambako ndiko alikozaliwa, bali ni wa Afrika Mashariki yote ambapo ametoa mchango wake katika kuendeleza dini ya kiislam.
Sheikh Ahmed amesema marehemu sheikh Al-bir aliweza kujifunza na kusomesha taaluma tofauti katika uhai wake, na wakati wote alikuwa akihimiza watu kusoma na kuendeleza taaluma wanazozipata kwa maslahi yao ya dunia na akhera.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu sheikh Al-bir mahali pema Paponi (Ammin).
No comments:
Post a Comment