Habari za Punde

Walioingiza unga mbovu wamepewa mwezi kuuondoa



Na Khamis Haji,OMKR
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amemtaka mfanyabiashara aliyeingiza Zanzibar tani 781 za unga wa ngano usiofaa kwa matumizi ya binaadamu ambao bado upo bandarini Malindi kuuondoa katika kipindi cha mwezi mmoja kuanzia jana.

Maalim Seif ametoa agizo hilo alipotembelea bandarini Malindi kwa ajili ya kupata maelezo ya utekelezaji wa agizo la serikali la kuondolewa unga huo.

Alisema unga huo lazima uondoke bandarini kwa sababu taasisi zilizofanya uchunguzi zimeugundua kuwa ni hatari kwa matumizi ya binaadamu, na kwa mujibu wa sheria bidhaa kama hizo hutakiwa zirejeshwe zilikotoka.  

“Natoa mwezi mmoja, kuanzia leo hadi Februari 13 wahusika mhakikishe unga huu umeondolewa Zanzibar,” aliagiza Maalim seif.

Unga huo wa ngano uliingizwa Zanzibar kutokea nchini Uturuki na kampuni ya Bopar Enterprises mwezi April mwaka jana, lakini tokea wakati huo bado haujaondolewa na hivi sasa umeanza kutoa harufu kali.


Maalim Seif  alieleza kuwa serikali ya Mapinduzi Zanzibar haina muhali katika suala la kulinda afya za wananchi, kwa sababu vyakula visivyofaa vinasababisha hatari kubwa kwa afya za binaadamu.

Katika ziara hiyo ya Maalim Seif bandarini hapo, kampuni ya Bopar pamoja na kampuni ya uwakala wa meli iliyoleta unga huo zilionekana kuvutana,huku kila upande ukiutupia lawama upande mwengine kuwa ndio unaostahili kubeba lawama.

Hata hivyo, Maalim Seif alisema lazima wahusika wawajibike kwa mujibu wa sheria katika kulinda afya za wananchi, lakini pia waondoe msongamano katika bandari hiyo, ambapo nafasi yalipo makontena 30 yenye unga huo inahitajika kuwekwa mizigo mingine.

Mrajis wa Bodi ya Chakula, Dawa na Vipodozi, Dk. Burhan Othman Simai ambaye alikuwepo katika ziara hiyo, alisema bodi hiyo imegundua kuwa unga huo haufai kwa matumizi ya binaadamu, na kwa mujibu wa sheria mhusika anapaswa kuurejesha ulikotoka.

Hata hivyo, alieleza kuwa pamoja na kwamba sasa ni muda mrefu tokea kutolewa maamuzi ya bodi kuhusu bidhaa hiyo, wahusika wameshindwa kutekeleza.

Aliwataka wafanyabiashara wote kuhakikisha wanaingiza bidhaa ambazo ni salama na hazitaleta athari zozote za kiafya kwa watumiaji wake.

Kamati ya Mawasiliano na ujenzi ya Baraza la Wawakilishi pia iliagiza unga huo uondolewe wakati ilipotembelea bandari hiyo mwezi Novemba.

Hivi karibuni tani nyengine 325 za mchele mbovu aina rainbow na kitumbo unaomilikiwa  na mfanyabiashara Mohammed Salum Alaiy ulingizwa nchini ukitokea nchini India na Srilanka.

Tayari Bodi ya Chakula, Dawa na Vipodozi imeshaagiza unga huo urejeshwe ulikotoka lakini hakuna hakika kama agizo hilo tayari limetekelezwa.

2 comments:

  1. Raisi anafanya nini Ikiwa Watu hao hawataki kutii Amri ya Bodi. Tunataka Kiongozi na Serikali itakayoheshimika.

    ReplyDelete
  2. Nyie mmewapa mwezi mmoja, Mhe Mwakyembe aipa meli masaa 24 iondoke kwa kuleta mafuta chini ya kiwango

    Tusubiri huo mwezi tuone!

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.