Habari za Punde

ZAA yashinda vigezo vya kimataifa utoaji huduma

Na Mwantanga Ame
MAMLAKA ya Viwanja vya ndege Zanzibar (ZAA) kwa mara ya kwanza imethibitishwa kushinda vigezo vya kimataifa katika utoaji huduma bora.

Hatua hiyo inakuja baada ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TCAA), kuufanyia ukaguzi uwanja wa ndege wa kimataifa wa Zanzibar na kuridhika kwa kufikia vigezo vinavyotakiwa kuwepo katika viwanja vya ndege duniani.

Akizungumza na Zanzibar Leo, Mkuu wa viwango katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume, Talib Mohammed Chum, alisema ZAA imepata cheti cha kiwango cha kimataifa baada ya kukidhi viwango muhimu vya kimataifa.

Alisema cheti hicho kinaifanya Tanzania kupata hadhi ya kimataifa katika viwanja vyake vitatu kikiwemo cha Kilimanjaro, Uwanja wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Karume.

Akitaja baadhi ya sababu ambazo zilichangia kupatikana kwa cheti hicho,alisema ni pamoja na kuimarika kwa usalama katika maeneo ya msingi ya uwanja huo zikiwemo sehemu ya mizigo na vifurushi.

Eneo jengine ambalo alilitaja kuimarika alisema ni lile linalohusu wafanyakazi kupewa taaluma juu ya utoaji wa huduma mbali mbali pamoja na kuwa na kamati za viongozi wanaosimamia utekelezaji wa kazi za msingi ndani ya uwanja huo na kuwepo gari ndogo zinazofanya kazi uwanjani hapo.

Alisema maeneo mengine yalihusu kuimarika huduma za zima moto kwa kuwa na magari ambayo yana uwezo wa kufanyakazi hiyo kwa saa 24, uwanja kuwa na taa na kuwepo kamati ya kuangalia usalama wa uwanja.

Eneo jengine ambalo alilitaja ni lile linalohusu utoaji taarifa za safari za ndege katika mashirika mbali mbali yanayotumia uwanja huo, pamoja na kuimarishwa mfumo wa uwekaji wa kumbukumbu za safari na kutolewa taarifa za safari kwa abiria wanaotumia uwanja huo.

Kutokana kuimarishwa kwa maeneo hayo Mkuu huyo wa viwango alisema kumeifanya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TCAA) ambayo ndio wakala wa Shirika la Viwango la Kimataifa la Viwanja vya ndege lenye Makao Makuu yake nchini Canada kuupa leseni ya kimataifa uwanja huo kuwa miongoni mwa viwanja vinavyotambulika duniani.

Alisema hapo awali walishindwa kupata hadhi hiyo kutokana na taasisi hiyo kuwa chini ya serikali, ambapo ilishindwa kupewa leseni kutokana na ukosefu wa shilingi milioni 40 za ada.

Alisema maeneo ambayo hivi sasa yanaimarshwa ni pamoja na kuimarisha mipaka ya uwanja huo,utoaji wa huduma bora na kuimarisha miundo mbinu ya majengo ya uwanjapamoja na kukuza kiwango cha elimu kwa watumishi wake.

Alisema kupatikana kwa cheti hicho, kutaiwezesha Zanzibar kwenda sambamba na sheria za matumizi ya viwanja vya ndege za Jumuiya za Afrika Mashariki kwani tayari inafuata kanuni ambazo zimo ndani ya makubaliano ya nchi wanachama.

Baadhi ya mabadiliko ambayo yameonekana kufanyika ndani ya uwanja huo ni pamoja kuongezeka mashine za kufanyia ukaguzi mizigo ya abiria na abiria, kuweko kwa chumba maalum cha abiria daraja la kwanza na kuimarishwa kwa usalama katika eneo la uwanja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.