Habari za Punde

Maalim Seif aonya kulazimisha chuki za Kidini. Asikitishwa matokeo mabaya kidato cha 4



Na Khamis Haji, OMKR
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema kinachoonekana kuna ajenda imetayarishwa ya kutaka kulazimisha chuki za kidini Zanzibar, licha ya kuwa Zanzibar ina historia ya dahari ya watu kuvumiliana na kuishi pamoja, licha ya kuwepo watu wa imani tafauti.
Aliwataka wananchi wote wawe macho na ajenda zinazolengwa kuwavuruga na waendelee kuishi kwa mshikamano na umoja kama ambavyo wamekuwa wakiishi.
Maalim Seif alisema hayo jana usiku alipokuwa akihutubia hafla ya Maulid ya Kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W), huko Mjini Kiuyu, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Alisema ajenda hiyo huenda imetayarishwa na  watu wenye nia mbaya ambao wameamua kuyatumia matukio ya kuuawa na kujeruhiwa viongozi wa dini, kujenga chuki kwa wananchi.
 “Ni jambo la kusikitisha kuna watu wenye nia chafu dhidi ya wananchi, ambao wameamua kuyatumia matukio haya kujenga chuki miongoni mwa Wazanzibari wenyewe kwa wenyewe”, alionya Maalim Seif.


Maalim Seif alisema vitendo vya kuuawa na kujeruhiwa viongozi wa dini Zanzibar ni mambo mageni na kwa miaka mingi Zanzibar imekuwa ni mfano bora wa uvumilivu wa kiitikadi za kidini, licha ya kuwa asilimia kubwa  ya wananchi wake ni waislamu.

Alieleza kwamba wingi wa waislamu Zanzibar haukuifanya ifunge milango kwa watu wa imani nyengine na kwa wakati wote wamekuwa wakiabudu kwa mujibu wa imani zao bila ya bughdha yoyote.

Alisema Katiba ya Zanzibar imeweka wazi haki ya mtu kuabudu kwa mujibu wa imani yake na uhuru wa mtu kuabudu umelindwa.

“Ni Sultani wa Zanzibar ambaye alikuwa Muislamu ndiye aliyetoa ardhi kwa ndugu zetu Wakiristo kujenga Kanisa. Juzi nilipo kwenda kutoa salamu za rambirambi kwa Baba Askofu Shayo, baada ya kifo cha Padri Mushi, aliweka bayana kuwa lililotokea lisihusishwe na tafauti za kidini,” alisema Maalim Seif.

Hata hivyo, alisema inasikitisha kuona wakati Rais Jakaya Kikwete katoa maelekezo uchunguzi wa kina ufanywe na Kamishna wa Polisi Zanzibar ameshaweka wazi kuwa uchunguzi unaendelea,baadhi ya viongozi na magazeti ya Tanzania Bara yanachochea chuki za kidini na kusema kuwa Zanzibar kuna ugaidi na kwamba serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inawabagua Wakristu.

Alisema hali hiyo inaonesha kuwa kuna ajenda imetayarishwa kutaka kulazimisha chuki za kidini Zanzibar, kwa sababu Tanzania Bara kumetokea matukio mabaya zaidi,lakini hayajahusishwa na ugaidi.

Alitoa mfano matukio ya kuuawa kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza,na kuchinjwa kwa Mchungaji huko Geita,kuwa ni mabaya kabisa, lakini hakuna hata chombo cha habari kimoja kilichohusisha matukio hayo na ugaidi.

“Nasema Zanzibar hakuna ugaidi, hakuna ugomvi wa kidini.Yanayotokea yametusikitisha sana, ni matokeo ya uhalifu wa kupindukia, linaloweza kufanywa lifanywe kuwanasa wahalifu hawa na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sharia,” alisema Makamu wa Kwanza wa Rais.

Aliwataka wananchi wote wa Zanzibar kwa wakati huu kuwa watulivu na wasitawaliwe na jazba na wala wasichokozane,pia wasikubali kuchokozeka.

Akizungumzia matokeo ya mtihani wa kidato cha nne yaliyotolewa hivi karibuni, alisema ni matokeo mabaya na ya kuliza,kwa sababu hayaoneshi mustakabali mwema kwa watoto katika maisha yao ya baadaye.

Alisema ni wakati muafaka Serikali, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Walimu na jamii nzima kujiuliza nini sababu ya matokeo hayo mabaya na kujiuliza pia nchi inaelekea wapi?

Maalim Seif alisema sasa si wakati tena wa kutupiana lawama, badala yake lazima pande zote zikae zijadili wapi pamekosewa, ili ufumbuzi uweze kupatikana na hali kama hiyo isitokee tena  siku zijazo.

Katika salamu za wananchi wa Kiuyu kwenye Maulid hayo yaliyojumuisha waislamu kutoka maeneo mbalimbali ya Pemba, Unguja na Dar es Salaam, walisema miongoni mwa malengo yao ni kuona umoja wa wananchi wote unaimarika. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.