Na Mwandishi maalum, Kenya
MAELFU ya Wakenya kutoka
dini na makabila tafauti jana walikusanyika katika viwanja vya Uhuru kuiombea
amani nchi hayo, siku tano tu kabla ya kuingia katika uchaguzi mkuu
utakaofanyika Machi 4.
Sala hiyo ambayo iliongozwa
na Mchungaji, David Owuor pia ilihudhuriwa na wagombea wote wa kiti cha urais,
isipokuwa Musalia Mudavadi.
Tofauti na mikusanyiko
mengine, katika ibada hiyo wagombea wote walikaa jukwaa moja na kuungana na
Wakenya kusali pamoja na baadae kuomba dua ya kuliombea taifa hilo.
Wagombea wote waliahidi
kukubali matokeo kama uchaguzi huo utafanyika kwa misingi ya uhuru na haki.
Mgombea urais kupitia chama
cha Narc-Kenya, Martha Karua aliwambia
Wakenya waliokusanyika katika viwanja hivyo kuwa atakubali kushindwa kwa lengo
la kudumisha amani na mshikamano wa Wakenya.
Alisema atafanya kila
analoweza kuhakikisha uchaguzi huo unakuwa wa amani na kuwaomba raia wote pamoja na wagombea
wengine kuhakikisha amani na utulivu inadumishwa nchini humo.
Kwa upande wake, Waziri
Mkuu, Raila Odinga alisema amani
itaendelea kudumishwa nchini Kenya kabla na baada ya uchaguzi na kuahidi kuwa
uchaguzi huo utakuwa huru.
Naibu Waziri Mkuu, Uhuru
Kenyatta alisema atakubali kushindwa kama rais atakaechaguliwa atashinda
kihalali.
Wakati huo huo, mgombea urais
kupitia muungano wa Amani,Musalia Mudavadi amewaonya Wakenya kutowachagua
wagombea wanaokabiliwa na kesi katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu (ICC)
akisema uhusiano wa Kenya na nchi za magharibi utaharibika kama wagombea hao
watachaguliwa kuiongoza nchi.
Mudavadi alisema Kenya iwe
tayari kukabiliwa na vikwazo vya kiuchumi ambavyo vitaathiri kasi ya ujenzi wa
uchumi wa taifa.
“Sina mamlaka ya kuzungumza
kwa niaba ya nchi za magharibi, lakini ninachowambia ni uzoefu nilionao kama
nchi hizi zitatuwekea vikwazo vya kiuchumi,” alisema Mudavadi.
No comments:
Post a Comment