Habari za Punde

MATOKEO KIDATO CHA 4. Wavulana watesa. · Watahiniwa 28,582 wazuiliwa matokeo. 240,903 wapata alama 0



Na Kunze Mswanyama, DSM

MATOKEO ya watahiniwa 28,582  ya kidato cha nne yamezuiwa baada ya kutolipiwa ada ya mitihani  huku wanafunzi 789 wakifutiwa matokeo kutokana na kufanya udanganyifu.

Akitangaza matokeo hayo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Prof. Shukuru Kawambwa,  alisema jumla ya watahiniwa 456,137 sawa na aslimia 95.44 walifanya mitihani hiyo iliyofanyika mwezi Oktoba kati ya wanafunzi 480,036 waliosajiliwa.

Hata hivyo,Waziri Kawambwa alikiri kuwa upungufu mkubwa wa walimu,vitabu na maabara ni moja ya vyanzo vikubwa vilivyosababisha wanafunzi wengi kushindwa kufanya vizuri katika mitihani.

Ni skuli mbili tu za serikali zilizoingia katika orodha ya skuli 20 bora  ambapo shule ya wasichana ya  St.Francis ya Mbeya imeshika nafasi ya kwanza kitaifa.


Skuli hizo ni pamoja na sekondari ya Kibaha ya mkoani Pwani na sekondari ya Mzumbe ya Morogoro  huku shule kumi zilizofanya vibaya zikiwa ni pamoja na Mibuyuni ya Lindi,Ndame ya Unguja na Mamndimkongo ya Pwani.

Waziri Kawambwa alisema,kutokana na ufaulu huo kushuka kulinganisha na mwaka jana,serikali imedhamiria kuboresha Idara za ukaguzi wa shule huku ruzuku ya shilingi 25,000 ikitolewa kwa kila mwanafunzi kwa mwaka ambapo asilimia 50 ya fedha hizo zinatazamiwa kununulia vifaa vya kufundishia na kujifunzia.

Kuhusiana na kufutwa kwa matokeo ya watahiniwa 789, Prof. Kawambwa alisema,serikali inadhamiria kuwachukulia hatua kali za kisheria ikiwa ni pamoja na kufungiwa kufanya mitihani inayoandaliwa na NECTA kwa mwaka mmoja na kuonya kuwa, udanganyifu wowote kwenye mitihani ni kosa kisheria.

Alibainisha makosa mbalimbali yaliyosababisha kufutwa matokeo hayo kuwa ni pamoja na watahiniwa kubainika kuwa na miandiko tofauti katika somo moja,kukamatwa wakiwa na karatasi zenye majibu, ubainika kuwa a mfanano usio wa kawaida na watu wanne wakikamatwa wakiwafanyia mitihani watahiniwa wengine.

Makosa mengine ni pamoja na watahiniwa kuandika matusi kwenye karatasi za majibu, kukamatwa na simu ndani ya chumba cha mitihani,watahiniwa kukamatwa wakibadilishana karatasi za majibu kwa lengo la kufanya udanganyifu.

 “Kwa mujibu wa kifungu namba 6 (2)(b) cha kanuni za mitihani,watahiniwa wote waliobainika kufanya udanganyifu katika mitihani au kuandika matusi hawataruhusiwa kufanya mitihani inayoendeshwa na NECTA kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia siku ya kutangazwa matokeo,” alisema Kawambwa. 

Aidha,alisema kitendo cha kuandika matusi kwenye karatasi za matokeo ni cha utovu wa nidhamu wa hali ya juu na serikali haitavumilia kitendo hicho,hivyo itaangalia hatua zaidi za kisheria za kuchukua dhidi ya watahiniwa hao.

Jumla ya watahiniwa 24 waliandika matusi kwenye karatasi zao za masomo mbalimbali kitendo ambachho ni kinyume  kwa mujibu wa kifungu cha 5 (13) cha kanuni za mitihani,kutokana na makosa hayo kanuni ya 6(2)(a) imetumika kufuta matokeo yao.


Jumla ya wanafunzi 1,641, wamefaulu kwa daraja la kwanza, 6,453 daraja la pili, 15,426 daraja la tatu na 103,327 wakifaulu daraja la nne na wengine 240,903 wakipata daraja la sifuri.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.