Habari za Punde

Waliomwagia tindikali Sheikh Soraga wakamatwa. Wamo pia waliompiga risasi Padri Amrose



Na Mwandishi wetu, Dodoma
WATU watatu wanashikiliwa kwa tuhuma za kumwagia tindikali Katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Suleiman Soraga.

Sheikh Soraga alimwagiwa tindikali mwezi Novemba mwaka jana wakati akifanya mazoezi katika viwanja vya Msumbiji karibu na skuli Nyerere Zanzibar.

Akijibu suali la Mbunge wa Dole, Silvester Masele Mabumba, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Pereira Ame Silima alisema pia watu wawili wanashikiliwa kwa kumpiga risasi Padri Ambrose Mkenda.
Padri Mkenda alipigwa risasi Disemba 25 mwaka jana wakati akiingia nyumbani kwake Mpendae.

Hata hivyo, alisema matukio yote mawili hayana uhusiano wowote wa  kidini.

Naibu Waziri huyo pia alisema viongozi wote wawili walipatiwa matibabu  kwa gharama za serikali.


Aidha alisema serikali haitavumilia machafuko yoyote yenye ishara za kidini na kwamba itachukua hatua kali dhidi ya makundi yanayofanya vurugu za kidini.

Aidha Pereira alisema serikali inaendelea kuyafanyia uchunguzi baadhi ya makundi ya kidini yanayojiingiza katika vitendo vya vurugu kufahamu kama yanapata ufadhili kutoka mataifa ya nje na pindi wakibaini hilo, watayafutia usajili makundi hayo.

Kuhusu mgogoro wa gesi mkoani Mtwara, Waziri Mkuu Mizengo Pinda amevitaka vyama vya siasa kuacha kuwachochea watu kufanya vurugu kwa kisingizio cha gesi.

Alisema alichokibaini mkoani humo ni wanasiasa kuwadanganya wananchi kuhusu rasilimali hiyo, hali iliyosababisha kufanya vurugu kubwa zilizopeleka hasara ya zaidi ya shilingi bilioni moja.

Hata hivyo, alisema serikali itawafidia wale walioharibiwa mali zao wakati wa vurugu hizo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.