Habari za Punde

Wanafunzi Arumeru wadai kuathiriwa na maji

 
Na Mahmoud Ahmad,Arusha.
 
Wanafunzi wa shule ya seminari ya Ailanga Junior seminary iliyopo wilaya ya Arumeru mkoani Arusha wanakabiliwa na tatizo la uhaba wa maji safi na salama shuleni hapo,ambapo wanalazimika kufuata maji umbali mrefu na kuyanunua kwa gharama kubwa kutokana na maji yanayopatikana katika eneo hilo kuwa na kiwango kikubwa cha kemikali ya floride ambayo huwaathiri afya zao.
 
Wakizungumza na Waandishi wa habari shuleni hapo,wanafunzi hao wamesema kuwa maji yanayopatikana katika visima vya shule na eneo la kata husika yana kiwango kikubwa cha floride ambayo huathiri mifupa yao na kuwapelekea kuumwa na wengine kupinda miguu hususan wakazi wa eneo hilo wamekuwa wakisumbuliwa na tatizo hilo.
 
Emaline Shuma na Rizick Samson ni wanafunzi wa kidato cha tatu katika shule hiyo wanaelezea athari za maji hayo ambayo mara nyingi wamekuwa wakiyatumia kufulia,kuoshea vyombo na kuoga,wamesema kuwa maji hayo yamekuwa yakibadilisha rangi ya meno na kuwapelekea maumivu ya mifupa katika miili yao tatizo ambalo linasababishwa na maji hayo.
 
“Wakati mwingine tumekuwa tukiumwa na magonjwa ya tumbo mfano Amoeba ambayo imekuwa ikiwasumbua wanafunzi wengi shuleni hapa wanaolazimika kutumia maji haya baada ya kukosa maji safi na salama hivyo tunaiomba serikali itusaidie tuweze kupata huduma ya maji safi itakayonusuru afya za wanafunzi wengi kutodhurika na maji haya yenye kiasi kikubwa cha floride” Timoth Samwel Mbise mwanafunzi wa kidato cha nne.

Kwa upande wake Mwalimu George Elia amesema kuwa maji yanayopatikana katika visima vya shule na kata hiyo kwa ujumla si mazuri kwa afya ya binadamu kutokana na kuwa na floride nyingi hivyo wanalazimika kuyafata maji umbali mrefu hadi kata ya Usa mjini na kuyanunua kwa gharama kubwa jambo linalosababisha kupanda kwa gharama za uendeshaji wa shule hiyo.
 
Akijibu Changamoto hiyo Mgeni rasmi katika mahafali ya kidato cha sita shuleni hapo ambaye ni Mkuu wa mkoa wa Dodoma Dr.Rehema Jonathan ameeleza kuwa tatizo la ukosefu wa maji halitachukua muda kupata suluhisho kwa kuwa shule hiyo iko karibu na hifadhi ya Meru inayosimamiwa na TANAPA ambapo kumekuwa na vyanzo vya maji kutoka katika hifadhi hiyo,hivyo ni muhimu mamlaka hiyo ikaisaidia jamii hiyo na shule.
 
Pia ameeleza kuwa ataifikisha changamoto hiyo kwa mkuu wa mkoa husika na serikali ili taitizo hilo liweze kupatiwa ufumbuzi ikiwa ni pamoja na tatizo la kutokuwepo kwa uzio kunakosababisha wakati mwingine wanyama kutoka hifadhi kuingia hadi ndani ya shule hiyo jambo ambalo linaweza kuhatarisha usalama wa wanafunnzi na mali za shule hiyo.
 
Hata hivyo Mwalimu mkuu wa seminari hiyo Bi.Lydia Mbise amesema kuwa shule hiyo inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vyumba vya madarasa vya kutosha na jingo la kulia chakula maarufu kama bwalo na kuongeza kuwa iwapo shule hiyo itakamilisha ujenzi wa maabara itaanza kuchukua wanafunzi wa michipuo ya sayansi kidato cha tano na cha sita.
 
Shule ya sekondari Ailanga Junior Seminary ni shule inayomilikiwa na Kanisa la Kilutheri Tanzania,shule hii ina jumla ya wanafunzi 450 ambapo kwa mwaka jana imeshika nafasi ya saba kikanda katika matokeo ya kidato cha sita,shule hiyo ilianzishwa tangu mnamo mwaka 2003 ikiwa na lengo la kutoa elimu bora kwa watoto wa kitanzania na kuwafundisha maadili mema katika jamii.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.