Habari za Punde

CHADEMA kutopokea wadandiaji

Na Mwandishi wetu
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema hakitawapokea wanachama wa vyama vyengine wanaoshindwa katika kinyang’anyiro cha kuwania uongozi kuelekea katika uchaguzi mkuu 2015.

Katika uchaguzi uliopita, chama hicho kilikuwa kimbilio la wanachama wa vyama vyengine, ikiwemo CCM, ambao walishindwa katika kinyang’anyiro cha kuwania ubunge.

Kauli hiyo itakuwa pigo kwa wanachama wa vyama vyengine, ambao wamekuwa wakikimbia chama hicho kupewa nafasi ya kugombea baada ya kushindwa katika hatua za mchujo ndani ya vyama vyao vya zamani.

Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Freeman Mbowe, alisema Chadema inahitaji watu waliopikwa na wanaofahamu misingi na mtazamo wa chama hicho na sio wale ‘wanaodandia’ kwa sababu tu ya kutaka uongozi.

Aidha alisema sera mpya ya majimbo itakiwezesha chama hicho kushika dola na kuongoza nchi kwa urahisi zaidi.

Alisema sera ya majimbo ni mkakati uliobuniwa na chama hicho kwa lengo la kusogeza madaraka kwa wananchi ili kushiriki kufanya maamuzi ya jinsi ya kuongoza nchi.

Alisema utamaduni, ambao umezoeleka nchini na ambao unatumiwa na serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni kuongoza nchi kutokea Dar es Salaam, hatua ambayo imeonesha kushindwa kuboresha hali ya maisha ya Watanzania wengi.

Alisema kwa kufuata sera ya majimbo, serikali ya CCM haiwezi tena kuwadhibiti viongozi wa Chadema isipokuwa watashtukia chama hicho kimeshika dola na kuongoza nchi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.