Na Said Ameir,Ikulu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameutaka uongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo kuchukua hatua za makusudi kuwaelemisha wananchi kuhusu matumizi ya ving’amuzi vinavyoendelea kutolewa na Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC).
Dk.Shein alitoa kauli hiyo alipozungumza na viongozi wa Wizara hiyo alipokagua matayarisho ya uwekaji wa mitambo ya digitali katika kituo cha ZBC Mkanjuni Chake Chake, Mkoa Kusini, Pemba.
Katika maelezo yake kwa Rais, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo,Dk. Ali Mwinyikai alisema kumekuwepo na changamoto nyingi tangu Shirila la Utangazaji la Zanzibar lilipoanza kutoa ving’amuzi kwa ajili matangazo ya digitali Zanzibar ambapo baadhi yake alizieleza kuwa zinatokana na wananchi wengi kutokuwa na uzoefu wa kutumia vifaa hivyo.
Dk. Shein alieleza kuwa malalamiko ya wananchi yanayohusu ving’amuzi kukosa matangazo au kukosa ishara (signal), uchache wa channeli pamoja na kukosekana kwa baadhi ya channeli wizara iyatolee maelezo ya mara kwa mara ili wananchi waelewe na kuondosha malalamiko.
“Lazima wizara muwe na vipindi vya mara kwa mara kuwaelemisha wananchi juu ya ving’amuzi kupoteza ‘signal’, uchache wa chaneli na kukosekana kwa baadhi ya chaneli,”aliagiza.
Rais alisema wananchi wanahitaji elimu hiyo kwa sababu “wako waliozoea kutumia ving’amuzi lakini wapo wengi ambao vifaa hivyo ni vipya kwao” hivyo wanahitaji elimu ya namna ya kuvitumia.
Dk. Shein aliutaka uongozi wa wizara ya habari kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha kuharakisha utaratibu kuweka studio mpya ya kisasa ambayo itatumika kutayarishia vipindi na kurushia matangazo.
Akizungumzia hatua ya uwekaji mitambo ya digitali kisiwani Pemba, Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Said Ali Mbarouk alisema ‘signal’ ya matangazo ya digitali imefika kisiwani Pemba Jumanne ya Machi 19 katika kituo cha Kichunjuu na inatarajiwa ifikapo tarehe 28 Machi itakuwa imefika katika kituo cha Mkanjuni hivyo kuenea kote kisiwani Pemba na kuifanya Zanzibar yote kuwa na mfumo wa Digitali.
“Matayarisho yanaendelea vyema na ving’amuzi vimeshawasili Pemba na tutaanza kuviuza rasmi kwa wananchi kesho Jumatano (jana),”alieleza Waziri huyo.
Kuhusu malalamiko ya wananchi kukosa baadhi ya chaneli hasa zile za michezo hasa mpira wa miguu, Waziri alieleza kuwa wizara yake inafanya jitihada kuzungumza na makampuni yenye haki ya kutoa matangazo hayo ili waweze kushirikiana na hatimae matangazo hayo yaweze kuwepo katika king’amuzi cha ZBC.
Awali akitoa maelezo kwa Rais, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dk. Mwinyikai alieleza kuwa usambazaji wa ving’amuzi unaendelea vizuri kisiwani Unguja lakini umekumbwa na changamoto nyingi ikiwemo malalamiko kuwa ving’amuzi ni vibovu lakini kilichogundulika ni kuwa wanachi wengi hawajavizoea.
“Wanapokosa ‘signal’wanarejesha au wanalalamika na kusema ni kibovu kumbe sio hivyo, wengine wanalalamikia kuwa chaneli ni kidogo kwa kuwa wanalinganisha na ving’amuzi vinavyotolewa na kampuni nyingine,”alieleza.
Dk. Mwinyikai alifafanua kuwa kukosa ‘signal’ mara nyingi husababishwa na kukosekana kwa umeme wa kutosha katika kituo cha Masingini Unguja kutokana na hali halisi ya tatizo la umeme lilivyo hivi sasa.
Mapema Waziri wa Ardhi, Makaazi Maji na Nishati, Ramadhan Abdalla Shaaban, alimhakikishia Dk. Shein kuwa tatizo hilo la umeme litamalizika mara baada ya kuanza kazi waya mpya wa umeme.
Wakati huo huo, Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA), imeeleza kuwa mradi wa ujenzi wa tangi la maji safi na salama unaoendelea Gombani unatarajiwa kumalizika mwanzoni mwa mwaka ujao na kuweza kuondoa tatizo la maji katika eneo kubwa la mji wa Chake Chake na vitongoji vyake.
Akitoa maelezo kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, Mkurugenzi Mkuu wa ZAWA, Dk. Mustafa Ali Garu alieleza kuwa kukamilika kwa mradi huo utahusisha ujenzi wa visima saba katika maeneo mbali mbali ya Wilaya ya Chake.
Visima hivyo vitachimbwa kupitia fedha za mkopo wa serikali kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Alisema ujenzi wa tangi hilo unaofanywa na kampuni ya Sinohydro kutoka China na mshauri mwelekezi ni Hydro plan kutoka Ujerumani, mradi huo unasaidia kwa kiasi kikubwa kuondokana na tatizo la uhaba wa maji katika mji wa Chake na vitongoji vyake.
Dk. Garu aliyataja baadhi ya maeneo yatakayofaidiaka na huduma hiyo ya maji mara baada ya mradi huo kukamilika ni Vitongoji, Miingani, Kisiwani kwa Bintiabedi, Ng’ombeni, Wambaa, Piki, Kambini, Mbuyu Mkavu, Mjanaza, Kambwi na maeneo mengineyo.Aidha, alieleza kuwa mradi huo utagharimu zaidi ya shilingi bilioni 13.
Mapema Dk. Shein alipokea taarifa ya Mkoa iliyosomwa na Mkuu wa Mkoa Kusini Pemba, Juma Kassim Tindwa taarifa ambayo ilieleza utekelezaji wa shughuli za serikali kuanzia mwezi Aprili hadi Disemba 2012.
No comments:
Post a Comment