Na Mwantanga Ame
KUTOKUWEPO Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imesababisha shughuli za uandikishaji wapiga kura wapya katika daftari la kudumu la wapiga kura, kushindwa kufanyika na kulazimika kusogezwa mbele hadi Tume hiyo itapoundwa.
Tume ya Uchaguzi Zanzibar, iliyosimamia uchaguzi Mkuu wa Zanzibar, Oktoba 2010, ilimaliza kazi zake rasmi Disemba 27 mwaka jana na Januari 1, 2013, ilikabidhi rasmi ripoti ya uchaguzi huo kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein.
Zoezi la uandikishaji wapiga kura waliotimiza masharti, lilitarajiwa kuanza mwishoni mwa mwiki ya mwisho wa mwezi huu.
Tume hiyo ambayo ilikuwa ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Khatib Mwinyichande, iliteuliwa na Rais mstaafu, Dk. Amani Abeid Karume.
Tume hiyo katika utawala wake iliweza kusimamia uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, na chaguzi ndogo nne, pamoja na kusimamia na kuendesha kura ya maoni ya kwanza katika historia ya Zanzibar kufuatia maridhiano ya kisiasa ya Novemba 5, mwaka 2009.
Akizungumza na Zanzibar Leo, Ofisa Uhusiano wa Tume hiyo, Idrisa Haji Jecha, alisema muda wa kuanza kazi za kuandikisha wapiga kura wapya zitashindwa kuanza kutokana na kukosekana kwa tume mpya.
Alisema tume ya uchaguzi kisheria ipo katika maeneo mawili tofauti, kiutawala na upande mwengine ndio inayoshughulikia kazi za usimamizi wa uchaguzi, baada ya kuwepo wajumbe wa Tume hiyo ambao huteuliwa na Rais.
Alisema kutokana na kutofanyika uteuzi wa wajumbe wa tume mpya, tume hiyo italazimika kushindwa na kazi za uandikishaji wapiga kura wapya, hadi pale uteuzi huo utapofanywa, kwa vile ndio yenye mamlaka ya kuidhinisha kazi hizo.
Alisema, tume iliyopo sasa ni ya kiutawala tu na kazi yake ni kuandaa taratibu za kazi kwa ajili ya kuwapatia wajumbe wa tume watakaochaguliwa,ili kutoa mapendekezo yao na baadae kurudishwa ngazi ya utawala wa kuyafanyia kazi.
Alisema kama tume mpya ingekuwepo ingeweza kuanza kazi zake za usajili wa wapiga kura wapya katika muda huo.
Alisema matayarisho ya kuanza kazi hiyo yamekamilika, ambapo kazi kubwa wanayokusudia kuianza ni kufanya usajili wa wapiga kura wapya ambao wanatarajiwa kufikia 200,000 hadi 250,000.
Aidha, alisema kazi nyengine wanayotarajia kufanyika ni kuziangalia kesi mbali mbali zikiwemo zinazohusu upoteaji wa kadi za wapiga kura ambapo tayari wamepokea maombi 558.
Kesi nyengine ambazo alizitaja ni zile zinazohusu watu waliohama kutoka eneo moja alilopigia kura uchaguzi uliopita, na kuhamia maeneo mengine, ambao wataweza kuzingatiwa baada ya kuwa na vielelezo sahihi.
Jecha alisema kazi hiyo itaenda sambamba na kuwashughulikia wananchi ambao walisajiliwa kuwa wapiga kura katika uchaguzi uliopita, lakini walishindwa kuchukua kadi zao hadi sasa.
Alisema idadi ya watu hao ni kubwa, na Tume itatoa vitambulisho hivyo, baada ya kupata vielelezo halisi kwa vile wananchi hao walioandikishwa walipewa risiti maalum kwa ajili ya kupewa kadi hizo.
ZEC inaendesha zoezi hilo, baada ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP), kutoa msaada wa dola za Marekani milioni 22.5 (sh. bilioni 36) kwa Tume ya taifa ya Uchaguzi (Nec) na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Mbali na UNDP, wafadhili wengine walioonyesha nia ya kusaidia katika utekelezaji wa mradi huo kupitia bajeti ya UN ni Norway, Sweden, Ireland, Finland, Canada, Uingereza, Umoja wa Ulaya (EU), Denmark, na Uswis watakaochangia kupitia mfuko wa pamoja wa wafadhili.
No comments:
Post a Comment