Na Husna Mohammed
SHIRIKA la Umeme Zanzibar (ZECO), limesema kuwa umeme wa uhakika Zanzibar utaanza kupatikana mwishoni mwa mwezi huu wa Machi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Gulioni, Meneja Mkuu wa shirika hilo, Hassan Ali Mbarouk, alisema mradi wa umeme wa uhakika Zanzibar uko katika hatua za mwisho.
“Nasikitika sana kuwaarifu wananchi kuendelea kustahamili na hivyo umeme wa uhakika utapatikana mwishoni mwa mwezi Machi mara baada ya kukamilika taratibu zilizobaki,”alisema.
Alizitaja kasoro ambazo zimesababisha kutokamilika mradi huo kuwa ni pamoja na kutokamilika kwa vituo vidogo vya umeme hasa kwa vifaa aina ya brakers ambavyo vimeonekana na hitilafu na vimerejeshwa nchini Ufaransa na vyengine vitawasili Machi 6.
Hata hivyo, alisema njia kuu za juu za umeme zinazojengwa na kampuni kutoka India zimeshakamilika na kwamba kilichobaki ni majaribio tu.
“Mradi wa waya wa baharini umekamilika ambao unafanywa na kampuni kutoka Japan,” alisema Meneja huyo.
Meneja mkuu huyo alisema majaribio kwa ajili ya umeme huo wa uhakika unatarajiwa kufanywa Machi 12 kwa muda wa saa 24 ambapo mara baada ya majaribio hayo huduma hiyo wakati wowote itaunganishwa katika laini kuu ya umeme kwa ajili ya kufanya kazi iliyokusudiwa.
Hata hivyo, alisema mradi huo ulitarajiwa kukamilika mwezi Septemba mwaka huu lakini kutokana na umuhimu wake kwa nchi, serikali iliwaomba wafadhili na kampuni zilizojenga mradi huo kukamilisha kabla ya kufikia mwezi huo.
Mradi huo wa umeme wa awamu ya pili umegharinu jumla ya dola milioni 64.9 ambapo kati ya hizo dola milioni 1.5 zimetolewa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na dola milioni 63.4 zimetolewa na Marekani ambao ni wafadhili wa mradi huo.
No comments:
Post a Comment