Azam FC, Tanzania Prisons vita vikali
Na Mwandishi Wetu
MABINGWA watetezi wa ligi kuu ya soka Tanzania Bara, Simba, leo watakuwa na shughuli pevu dhidi ya Kagera Sugar katika uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba katika mfululizo wa mechi za ligi hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya simu Vodacom.
Mbali na pambano hilo linalotarajiwa kuwa la kukata na shoka, mechi nyengine itachezwa katika uwanja wa Chamazi Complex, ambapo Azam FC inayoshika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo, itaikaribisha Tanzania Prisons ya Mbeya.
Simba, ambayo kimtazamo imeshapoteza matumaini ya kulibakisha taji kwenye himaya yake kutokana na kuzidiwa kwa tafauti kubwa ya pointi na watani wake wa jadi Yanga, itakuwa ikisaka ushindi kwa udi na uvumba, ili angalau ifufue matumaini ya kuipiku Azam na kushika nafasi ya pili mwisho wa msimu.
Kabla ya mchezo wa leo, wekundu hao walishacheza mechi 19 na kushinda tisa, kutoka sare saba na kupoteza mechi tatu, ikiwa na pointi 34, katika nafasi ya tatu.
Kocha Mfaransa anayeinoa timu hiyo Patrick Liewig, anatarajiwa kuwatumia wanandinga wake wote muhimu, ingawa ameamua kumuacha Mwinyi Kazimoto
nje ya kikosi kilichokwenda Kagera.
Hata hivyo, ushindi kwa timu hiyo hautakuwa rahisi, kwani kocha mkuu wa Kagera Sugar Abdallah Kibaden ‘King Mputa’, amesema hakuna kitu kikubwa anachotaka kuifanyia timu yake kama kuifunga Simba, ambayo aliwahi kuchezea kwa mafanikio makubwa kwenye miaka ya 1970/1980.
“Itakuwa fahari kubwa kwangu kushinda mechi hii, na nimejiandaa kupeleka kilio Msimbazi, wachezaji wangu wako tayari ni wanajua ninachotaka wafanye kesho (leo)”, alisema kwa kujiamini Kibadeni.
Ukiondoa mchezo huo, pambano kati ya Azam na maafande wa Tanzania Prisons, litakuwa na mvuto wa aina yake, kwani linakutanisha timu mbili zenye uwezo wa kutandaza kabumbu safi.
Bila shaka, matajiri wa Azam, ambayo ndiyo timu pekee kwa Tanzania mwaka huu, iliyobaki kwenye michuano ya klabu barani Afrika, watataka kuendeleza wimbi la ushindi ili kuifukuzia Yanga inayotanua kileleni kwa muda mrefu sasa.
Azam inayofundishwa na Muingereza Stewart John Hall na ikijivunia wachezaji kadhaa nyota wa kigeni, imekuwa gumzo kubwa nchini na kuanza kufuta mawazo mgando ya mashabiki ya U-Simba na U-Yanga, na tayari imecheza mechi 19, ikiwa na pointi 37 katika nafasi ya pili.
Nao walinzi wa wafungwa, Tanzania Prisons, pamoja na kuwa katika nafasi ya 11 kwa pointi 22, si timu ya kubeza kwani ina uwezo wa kubadilisha matarajio ya timu pinzani ndani ya dakika 90.
No comments:
Post a Comment