Na Abdi Suleiman, Pemba
WAKATI ligi daraja la kwanza Taifa Pemba, ikiwa imebakisha michezo mitatu kwa kila timu, klabu ya Kizimbani ya Wete, tayari imekata tiketi ya kurudi tena kucheza ligi kuu ya Zanzibar msimu wa 2013/2014.
Katika ligi hiyo inayoshirikisha timu 15 Kizimbani imeshatia kibindoni pointi 60, kukiwa hakuna timu itakayoweza kufikia idadi hiyo mwisho wa michuano hiyo.
Juzi, timu hiyo iliitandika African Kivumbi ya Mwambwe goli 1-0 na kufikisha pointi hizo 60 , katika mchezo uliopigwa dimba la Gombani.
Katika mchezo huo ulioshuhudiwa pia na Mwakilishi wa Jimbo la Kiwani Hija Hassan Hija akiwaongoza mashabiki wa African Kivumbi, timu zote zilicheza kwa ushindani mkubwa na kutoa burudani mwanana kwa watazamaji.
Bao pekee lililopeleka kilio katia kijiji cha Mwambe, liliwekwa nyavuni na Abdullatif Omar katika dakika ya 16 na kufuta ndoto za Kivumbi kumfurahisha Mwakilishi wao kwa kutoka na ushindi.
Huku Kizimbani ikijikusanyia pointi 60, African Kivumbi na FSC zinaendelea kukabana koo katika nafasi ya pili, zote zikiwa na pointi 47.
Na katika mchezo mwengine wa ligi hiyo, mizinga ya maafande wa Hard Rock ikashindwa kufyatuka bada ya kutiuwa maji kwa kuchapwa goli 1-0 na Konde Star, goli lililofungwa na Mussa Hamad.
Nayo Al Jazira ikaikatisha matumaini ya kubakia katika ligi hiyo, timu ya Coast Boys kwa kuirovya magoli 5-3.
No comments:
Post a Comment