Na Mwantanga Ame
MASUALA ya kisiasa ni moja ya sababu zilizosababisha kusambaratika asasi nyingi za kiraia nchini.
Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, mama Asha Seif Iddi, aliyasema hayo wakati akizindua rasmi jumuiya ya Vijana ya Kibweni (Kibweni Youth Organization), katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), kampasi Beitras mjini Zanzibar.
Jumuiya hiyo, inakusudia kufanya kazi za kusimamia mazingira ya bahari juu ya utupaji wa taka zenye sumu, elimu kwa jamii juu ya watoto wa kike kujiepusha na vitendo vya upataji wa mimba za utotoni, elimu ya kupambana na maradhi ya ukimwi na kuwasaidia wanafunzi namna ya kujiandaa na mitihani.
Alisema ni lazima jumuiya hiyo ione umuhimu wa kujikuza ili iweze kufanya kazi zake vizuri, kwani hivi sasa kuna jumuiya nyingi zilizoundwa lakini zimebakia majina baada ya kusambaratishwa na siasa.
Alisema inasikitisha kuona Zanzibar imebahatika kuwa na NGO’s nyingi, lakini baadhi yake zinakosa kuwa na mafanikio jambo ambalo ni tofauti na taasisi za aina hiyo kwa Tanzania Bara.
Alisema sababu kubwa ambazo zimeonekana kuchangia kujitokeza matatizo ya aina hiyo, ni pamoja na mitazamo ya kisiasa ambayo inaonekana kuvuruga shughuli za jumuiya hizo.
Kutokana na hali hiyo,alisema ni vyema jumuiya hiyo kuutambua udhaifu huo na kuhakikisha hawatoi nafasi kwa watakaothubutu kuja na mawazo ambayo yatayoonesha misimamo ya kisiasa ndani ya shughuli za jumuiya hiyo.
Alisema baadhi ya shughuli zinazokusudiwa kufanywa na Jumuiya hiyo ni muhimu kwa Zanzibar, kutokana na kuhitaji msaada kutoka katika maeneo mbali mbali hasa yanayohusu jamii.
Aliwataka viongozi wa jumuiya hiyo, kufikiria kuwahusisha wazee wa eneo hilo kusaidia maarifa kutokana na sehemu kubwa ya wanachama wake kuwa ni vijana.
Mbunge wa Jimbo la Bububu,aliwapongeza vijana wa shehia hiyo, kwa kuanzisha NGO’s hiyo kwani itaweza kuwa msaada mkubwa wa vijana.
Mapema Katibu wa jumuiya hiyo,Kassim Salum, alisema ipo kwa kwa ajili ya kukuza maendeleo ya Zanzibar na ni vyema kwa viongozi wa serikali kuendelea kuiunga mkono.
Katika uzinduzi huo iliendeshwa harambee ambapo jumla ya shilingi milioni 3.1 zilikusanywa ambapo mama Asha alichangia shilingi 1,000,000.
No comments:
Post a Comment