Na Husna Mohammed
MGOGORO mkubwa umezuka kati ya mwekezaji wa kiwanda cha sukari na wananchi wa maeneo ya Mahonda kutokana na mwekezaji huyo kuamuru kuvurugwa mashamba ya wananchi waliolima katika shamba la miwa linalomilikiwa na mwekezaji wa kiwanda hicho.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi kwa masharti ya kutotajwa majina, wananchi hao baadhi yao walisema mashamba hayo wamepewa na serikali ya wilaya lakini cha kushangaza kumekuwa kukitokea migogoro ya mara kwa mara na mwekezaji wa kiwanda hicho.
“Sisi tumepewa na mara zote tumekuwa tukilima lakini cha kushangaza tunaona vitisho kila siku na mara hii mpaka tumepanda ndio yanaingizwa matrekta katika mashamba yetu,” alisema mkulima mmoja wa eneo hilo.
Aidha imebainika kuwa kuna baadhi ya wananchi wameyavamia mashamba ya mwekezaji huyo bila ya kukabidhiwa na serikali ya wilaya.
“Tuko wengi ambao tumeamua kulima katika mashamba haya baada ya kuona kuwa mashamba haya yamekaa bure na sisi tunahitaji maeneo ya kilimo ili kutusaidia katika maisha yetu ya kila siku,” aliongeza.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja, Khamis Makame Jabir, alikiri kuharibiwa kwa vipando kwa baadhi ya wakulima waliovamia shamba hilo.
Hata hivyo, alisema wawekezaji hao walifika ofisini kwake majira ya saa 7 mchana juzi (Jumanne) kwa ajili ya makubaliano yaliyoambatana na masharti maalumu dhidi ya wakulima waliovamia mashamba hayo kwa ajili ya kilimo cha mpunga.
Aliyataja masharti hayo ni pamoja na mwekezaji huyo kustahamili hadi hapo wakulima hao watakapovuna mipunga yao.
“Kwa kweli mwekezaji huyu ni msikivu sana kwani ameshatukubalia mambo mengi lakini pia ameona umuhimu wa mashirikiano kati yake na wananchi wanaozunguka kiwanda hichi na ndio maana akawaachia hadi hapo watakapovuna mazao yao,” alisema.
Sambamba na hilo lakini Mkuu huyo wa Wilaya alisema awali serikali ya mkoa ilimuomba mwekezaji huyo ekari 1,100 na baadae ekari 40 kwa ajili ya kuwapa wananchi kujishughulisha na kilimo.
Mapema wiki iliyopita Meneja Mradi wa kiwanda hicho kilichopewa jina la Export Trading Group, Tushar Mehta, alisema kwamba licha ya kutoa ekari 150 kwa wananchi lakini amebakiwa na ekari 4,400 kati ya ekari 6,529 za kiwanda hicho.
Aidha alisema kuwa nyumba 172 zinazomilikiwa na kiwanda hicho ni nyumba nane tu ndizo alizokabidhiwa jambo ambalo ni kinyume na mkataba kati yake na serikali.
Sambamba na hilo pia mwekezaji huyo aliiomba serikali kufuta deni la umeme la shilingi milioni 52 na baadae kiwanda hicho kianze hatua mpya ya kuanza uzalishaji.
Hali hiyo huenda ikazorotesha upandaji miwa katika shamba hilo ambao ulitarajiwa kuanza mwezi ujao.
Katika ziara yake kiwandani hapo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi aliahidiwa kuwa uoteshaji wa miwa utaanza hivi karibuni na uzalishaji sukari utaanza mwezi Oktoba.
No comments:
Post a Comment