Na Kunze Mswanyama,Bagamoyo
KATIKA hali ya kushangaza,mwalimu mmoja wa shule ya sekondari ya Dunda iliyopo Bagamoyo,ameitaka kamati ya Katiba,Sheria na Utawala kuondoka na wanafunzi wote wa skuli hiyo,kutokana na wengi wao kuwatukana walimu wao na kuwatishia kwa silaha huku mamlaka za juu zikilifumbia macho suala hilo.
Mwalimu huyo ambaye aliamua kuvunja ukimya mbele ya kamati hiyo inayoongozwa na Dk.Pindi Hazara Chana,aliamua kueleza yote ya moyoni hali iliyoifanya kamati hiyo kuingiwa na simanzi.
Akielezea hali hiyo ya kutishiwa maisha na kutukanwa ambayo sasa imekuwa ni jambo la kawaida kwa walimu hao kutendewa na wanafunzi wao,mwalimu huyo aliiambia kamati hiyo,”nawaomba wabunge muondoke na zigo lenu hilo,kila siku tunaishi kwa woga unaosababishwa na wanafunzi wetu na halmashauri imekaa kimya tu japo inafahamu kila kitu,”alisema mwalimu huyo.
Wakati anaelezea hayo, wajumbe wote wa kamati hiyo walikaa kimya kwa utulivu mkubwa hali iliyomfanya mwalimu huyo kufikisha ujumbe wake ambao haikujulikana kama aliagizwa na wakubwa zake kusema hayo ama ni utashi wake tu kutokana na makubwa hayo yaliyomsibu.
Baada ya kusema hayo,zamu ikawa ni ya Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, William Ngeleja kueleza msimamo wa kamati ambapo alimpa nafasi mwalimu huyo kuiomba kamati hiyo iwafanyie nini,ndipo aliposema:
“Nawaomba mje kama walimu hapa kwa mwezi mmoja muone namna tunavyokimbizwa na mapanga,matusi na nyimbo ambazo wanafunzi huamua kuziimba kama hawalitaki somo lako,nyie mmekaa huko juu mnasema walimu hatufundishi,tunateswa na watoto wenu hawa,”alidai mwalimu huyo wa kike.
Aliongeza kuwa,”najuta sana kuileta shahada yangu katika mkoa huu ambao wazazi na wanafunzi hawajui umuhimu wa shule,kusoma na kufaulu,hali hii sijaizoea kabisa maana kwetu sisi hatuna utovu mkubwa wa nidhamu kama unaooneshwa na wanafunzi hawa wa Bagamoyo”.
Mwalimu huyo ambaye aliamini ujio wa kamati hiyo ni kusikiliza kero zao,alizidi kusema kuwa,anamshangaa Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Samuel Sarianga kukaa kimya bila kuchukua hatua zozote.
Baada ya kumalizika kwa zamu ya mwalimu huyo kuiomba kamati hiyo iwafanyie hayo,zamu ikawa ni ya Mwenyekiti Dk.Pindi ambaye alitumia mamlaka waliyopewa kumuagiza Mkurugenzi huyo kuhakikisha anashughulikia kero hiyo ili kutia hamasa walimu hao waliokwishakata tamaa ya kazi ya ualimu.
“Mkurugenzi,nakuomba sana ushughulikie kero hiyo na nyingine zilizotajwa hapa,tena itendee haki kamati hii ambayo kwanza ilikuja kwa mengine lakini imekutana na mengine ambayo pia ni muhimu,shule hii iko kwenye Jimbo la Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi,nasi tutamwambia lakini timizeni wajibu wenu kwanza,”aliagiza mwenyekiti huyo.
Shule hiyo ya Dunda imejengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa kushirikiana na jamii ya kijiji hicho ambapo hadi juzi kamati hiyo ilipotembelea, haikuwa na vifaa vya ofisini licha ya kuwa na majengo mazuri.
Akijibu hali hiyo,Mkurugenzi Mkuu wa TASAF, Ladislaus Mwamanga alisema kwenye bajeti yao waliweka ununuzi wa vifaa vya ofisini lakini kutokana na ushiriki mdogo wa wananchi,waliamua kupeleka fedha hizo kwenye ujenzi hivyo baada ya majengo kukamilika hakukuwa na fedha za vifaa.
No comments:
Post a Comment