Na Mwantanga Ame
MKE wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, mama Asha Seif Iddi, amewataka wanachama wa kikundi cha ushonaji cha Hatubaguani cha Jimbo la Kitope, kuthamini mchango wa mafunzo wa kuwapatia ujuzi utakaochangia kupata ajira na kuondokana na umasikini.
Aliyasema hayo jana wakati akifunga mafunzo ya ushonaji kwa kikundi hicho, katika ukumbi wa ofisi ya Jimbo hilo Kinduni, wilaya ya kaskazini ‘B’ Unguja.
Alisema dhamira ya viongozi wa Jimbo hilo ni kuona vijana walioshindwa masomo yao, wanabuni njia mbadala za kujiletea maendeleo ili kupambana na tatizo la umasikini, na ndio maana wameamua kujitolea kuwapa mafunzo yatayowajengea uwezo.
Alisema vijana wengi hivi sasa wamekosa njia mbadala za kuwasaidia namna nzuri ya kukabiliana na maisha baada ya kumaliza masomo, na ndio maana Mbunge wa Jimbo hilo, Balozi Seif Ali Iddi ameamua kuanzisha mafunzo hayo.
Alisema kazi kubwa ambayo wananchi wa Jimbo wanapaswa kuifanya ni kushiriki katika mafunzo hayo kwani ndio njia pekee itayoweza kubadili maisha yao.
Alisema mengi ya majimbo hivi sasa yamekuwa na mahitaji makubwa ya vijana juu ya kukosa ajira, na mpango ulioanzishwa wa kutoa mafunzo ya ushoni kwa Jimbo hilo ni sehemu muhimu ambayo itawasaidia wananchi kupambana na umasikini.
Hata hivyo, Mama Asha, aliwataka wanakikundi hao kutokimbia mitihani baada ya kupokea taarifa za baadhi yao kuamua kukimbia mitihani jambo ambalo limewasababishia kutokamilisha mafunzo yao vyema.
Mapema Katibu wa Jimbo hilo, Khamis Khamis aliupongeza uongozi wa Jimbo hilo kwa kuamua kuanzisha mafunzo hayo kwani yataweza kuwasaidia vijana kukabiliana na hali mbaya ya maisha.
Nae Mwenyekiti wa kikundi hicho, Sichana Said Haji, alisema mafunzo hayo ni muhimu kwa wananchi wa Jimbo hilo kwani yatawasaidia kukabiliana na hali ngumu za maisha zinazowakabili hivi sasa.
Nae Mkurugenzi wa taasisi ya ushonaji ya Magomeni, Rashid Makame Shamsi, alishauri juu ya kuwepo mpango madhubuti utakaoweza kutoa hamasa kwa wananchi wa Jimbo kuyakubali mafunzo hayo kwani baadhi yao hawayapi uzito unaostahili.
No comments:
Post a Comment