Na Mwandishi wetu
RAIS mpya wa China,Xi Jinping anatarajiwa kuwasili nchini mwanzoni mwa wiki ijayo kwa ziara rasmi ya kiserikali.
Hiyo itakuwa ziara ya kwanza kwa kiongozi huyo tokea achaguliwe kuliongoza taifa hilo linalokua kiuchumi.
Akiwa nchini pamoja na mambo mengine Rais Jinping atafungua jengo la ukumbi wa mikutano wa kimataifa la Julius Nyerere Convertion Centre lililopo jijini Dar -es -Salaam linalomilikiwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, John Haule wakati wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa kimataifa walipotembelea jengo hilo ili kuona maendeleo ya ujenzi.
Haule alisema ujenzi wa ukumbi huo ni matunda ya mahusiano mazuri ya ushirikiano yaliyopo baina ya serikali ya China na Tanzania kwa makubaliano maalum ikiwa ni kama msaada na mkopo nafuu usio na riba ambao utalipwa kwa awamu mbili tofauti.
“Ukumbi huu ni wa kisasa,utatumika kama sekta ya utalii na biashara na utasaidia kuliingizia taifa fedha za kigeni kwani una sehemu kubwa ya kuegesha magari 222, chumba cha habari,mkahawa,ofisi za wazi na maktaba ndogo,”alisema Haule.
Aidha alisema ziara ya Rais Xi Jinping ni kuimarisha mahusiano baina ya Tanzania na China na kueneza sera ya mambo ya nje kwa kipindi chote cha utawala wake atakachokuwa madarakani.
No comments:
Post a Comment