Habari za Punde

Serikali yatakiwa kuchukua hatua tatizo la kufeli wanafunzi mtihani wa kidatu cha nne

Na Miza Kona, Maelezo 03-03-2013
WANAWAKE nchini Zanzibar, wameitaka serikali kulichukulia hatua tatizo la kufeli wanafunzi wengi katika mtihani wa kidatu cha nne mwaka jana na kulipatia ufumbuzi wa kudumu ili lisijirudie.
Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Wanawake wa Chama cha Wananchi CUF Wilaya ya Mjini, Mpaji Khamis katika mkutano wa hadhara uliofanyika jana Machi 2, 2013 katika uwanja wa Urafi SC Kwamtipura.
Alisema matokeo mabaya ya mtihani huo yamewatia majonzi makubwa wanawake nchini, ambapo asilimia kubwa ya wanafunzi wameanguba vibaya hali itakayochangia kuwarejesha nyuma kimaendeleo.
Aidha alisema wanawake ndio walezi hivyo wanaona uchungu mkubwa kutokana na matokeo mabaya ya watoto wao ambao waliwagharamia kwa kiasi kikubwa na hatima yake hawakupata kitu.



“Kilio chetu wanawake watoto wetu wanafelishwa, wanadhalilishwa sisi ndio wazazi tunaona uchungu watoto wamefeli vibaya sana tumegharamika nini tatizo tunaomba lichukuliwe hatua ili upatikane ufumbuzi”, alieleza bi Mpaji.
Nae mwakilishi jimbo la Mji Mkongwe Ismail Jussa Ladhu amesema hakuna jamii ya watu wanaojali nchi yao wakakubali kutawaliwa hivyo wazanzibari washikamane na kuungana kwa pamoja ili kuweza kuijenga nchi .
Alisema Zanzbar ni nchi ya biashara ambayo ina rasilimali nyingi itakayoweza kujiendeleza kiuchumi na vijana wake kuweza kupata ajira hivyo ipo haja ya kupata uhuru wake kamili wa kuweza kuamua na kujitawala bila ya kuingiliwa katika maamuzi yake.
“Zanzibar endapo itapata mamlaka yake kamili vijana wengi wataweza kupata ajira kutokana na biashara na rasilimali zake ziliomo na kuondoa wimbi kubwa la vijana wasio na ajira, ” alifahamisha.
Aidha alieleza muungano ni mzuri iwapo wananchi watakubaliana na kuweka maamuzi ya pamoja ambayo yataweza kuleta maendeleo katika pande mbili.
“Muungano sio kitu kitu kibaya ikiwa watu wataweza kukubaliana na kwenda pamoja katika kuleta maendeleo katika nchi, ” alieleza

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.