Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KOCHA wa Simba Patrick Liewig, amemtema kiungo Mwinyi Kazimoto miongini mwa wachezaji walioondoka jana kwenda Bukoba kwa ajili ya mechi ya ligi kuu dhidi ya Kagera Sugar, itakayochezwa kesho katika uwanja wa Kaitaba.
Hayo yamebainika baada ya wachezaji watano wa timu hiyo waliokuwa katika timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars, kuondoka jijini Dar es Salaam kwa ndege kwenda Bukoba jana asubuhi kuungana na wenzao waliotangulia huko juzi.
Ofisa Habari wa Simba Ezekiel Kamwaga, amemwambia mwandishi wa habari hizi kuwa, Kazimoto hayumo katika mipango ya kocha kwa sasa.
Wachezaji watano walioondoka jana baada ya mechi ya Taifa Stars na Morocco kusaka tiketi ya fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini Brazil, iliyochezwa juzi, ni kipa Juma Kaseja, mabeki Nassor Masoud, Shomary Kapombe na viungo Amri Kiemba na Mrisho Ngassa.
Tayari wachezaji wa Simba ambao hawakuwemo Taifa Stars, wapo Bukoba tangu juzi kwa ajili ya mchezo huo wa ligi kuu.
Aidha, Kamwaga alisema wachezaji wengine wawili waliokuwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Uganda, The Cranes kilichomenyana na Liberia juzi, kipa Abbel Dhaira na kiungo Mussa Mudde nao wataungana na timu moja kwa moja Bukoba.
Simba ambayo tayari imepoteza mwelekeo wa kutetea ubingwa wake kutokana na kuzidiwa pointi 14 na wapinzani wao wa jadi, Yanga wanaoongoza kwa pointi 48, inapigana kuhakikisha japo inakuwa ya pili kwa kuipiku Azam iliyo katika nafasi hiyo kwa pointi 37, huku wekundu hao wakiwa na pointi 34.
No comments:
Post a Comment