Habari za Punde

Stars kazi moja

 
 Inaivaa Morocco kusaka fainali za dunia Brazil 2014
 
Na Salum Vuai, Maelezo
 
TIMU ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, leo inashuka uwanja wa Taifa Dar es Salaam, kumenyana na Morocco, kwenye mechi ya kundi C kanda ya Afrika, kusaka tiketi ya fainali za Kombe la Dunia mwaka ujao zilizopangwa kufanyika nchini Brazil.
Kikosi cha Morocco, Lions of the Atlas, kiliwasili jijini Dar es Salaam juzi mchana, tayari kwa mpambano huo wa leo dhidi ya wenyeji Taifa Stars utakaoanza saa tisa mchana.
Wachezaji wa Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, wamekuwa kambini katika hoteli ya Tansoma, tangu Machi 17, mwaka huu, kujiandaa na mchuano huo unaotarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua.
Ili kujiwekea mazingira mazuri ya kunyakua tiketi ya fainali za Rio De Janeiro mwakani, Stars ni lazima ishinde leo, huku ikiomba matokeo kati ya Ivory Coast na Gambia yawe kwa manufaa ya Tanzania.

Stars inashika nafasi ya pili katika kundi C ikiwa na pointi tatu kabla mchezo wa leo, nyuma ya Ivory Coast yenye pointi nne.

Kama Tanzania itaweza kuongoza katika kundi lake, itaingia kwenye kumi bora ambako kutachezwa tena mechi za mtoano kupata timu tano kati ya 40 kutoka bara la Afrika, zitakazokwenda Brazil mwaka 2014.
Akizungumzia mchezo huo, kocha wa Taifa Stars Kim Poulsen, amesema ili kushinda na kutia mikononi pointi tatu muhimu, watacheza kwa kushambulia tangu mwanzo, lakini bila ya kusaahau kulinda lango lao lisihujumiwe.
Poulsen alitumia zaidi ya saa moja katika programu yake ya mazoezi siku ya Alkhamisi, kuwapa wachezaji wake mbinu za kufanikisha lengo hilo, ikiwa pamoja na kufanya mazoezi ya kupiga penelti.
Hata hivyo, kiungo mshambuliaji wa timu hiyo Khamis Mcha ‘Viali’, huenda atawakosa Waarabu wa Morocco, kutokana na kukabiliwa na maumivu ya nyonga.

Wachezaji wanaotarajiwa kuanza mchezo huo, ni; mlinda mlango
Juma Kaseja, mabeki Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, Aggrey Morris na Kelvin Yondani, pamoja na viungo na washambuliaji Frank Domayo, Mrisho Ngassa, Salum Abubakari, Mbwana Samatta, Amri Kiemba na Mwinyi Kazimoto.

Morocco itakuwa bila ya mshambuliaji wake nyota Marouane Chamakh, huku kocha wake Rachid Taoussi akipania angalau sare ili kurudisha imani ya kufuzu kwa kuwa bado wana baadhi ya mechi nyumbani.
Wachezaji wengine wa timu hiyo waliokuja ni Nadir Lamyaghri, Anas Zniti, Yassine Bounou, Younnnes Bellakhadar, Abdellatif Noussair, Abderrahim Achchakir, Zoheir Feddal, Younnes Hammal, Zakarya Bergdich, Abdeljalil Jbra na wengine kadhaa.
 
 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.