Habari za Punde

ZFA yajifungia Pemba kuzuia mapinduzi

 
Na Mwandishi Maalum, Pemba
 
BAADA ya kuwepo mwelekeo wa kuvunjwa uongozi wa Chama cha Soka Zanzibar, chama hicho kimeanza mikakati ya kujipanga upya ili kuzuia hali hiyo isitokee.
Uchunguzi wa gazeti hili uliofanywa Unguja na Pemba, umegundua kuwa tangu vikao vya wadau na Waziri anayeshughulikia michezo Said Ali Mbarouk wiki iliyopita kuonesha kuwa ZFA haikuibaliki, viongozi wa chama hicho wamekuwa wakihaha kutafuta njia ya kunusuru nafasi zao za uongozi.
Ili kujaribu kuzuia mapinduzi hayo yanayonukia, jana kutwa viongozi waandamizi wa chama hicho kutoka Unguja na baadhi ya wajumbe wa kamati tendaji, walikuwa wamejifungia katika hoteli ya Pemba Misali Chake Chake, kujadili kwa kina maelezo ya Waziri Mbarouk, alipozungumza nao Machi 15, ofisini kwake.
Uchunguzi wetu umebaini kuwa, Makamu wa Rais wa ZFA Unguja Haji Ameir, aliwaongoza wajumbe wengine watano na kuondoka kwa ndege mapema asubuhi, na kufikia hotelini hapo moja kwa moja kuanza kikao hicho, na kamati tendaji nzima ya ZFA kisiwani Pemba.
Mbali na Ameir, wengine waliokuwemo kwenye msafara huo ulioondoka kimyakimya, ni Katibu Mkuu wa ZFA Kassim Haji Salum, Suleiman Mahmoud Jabir, Salum Msabah, Masoud Attai na Mwanasheria wa chama hicho Abdallah Juma Mohammed.
Mmoja wa wajumbe wa kamati tendaji ya ZFA Pemba, alimdokeza mwandishi wa habari hizi kuwa, hatua hiyo imefuatia kushtushwa na maoni ya wadau wengi wa soka nchini mbele ya Waziri Mbarouk, kwamba hakuna dawa ya kumaliza malumbano zaidi ya kuuvuja uongozi wa chama hicho na kuunda kamati ya muda.
Katika hatua nyengine, uongozi wa juu wa chama hicho, umepanga kukutana na waandishi wa habari wa Unguja kesho wakati wa saa nane mchana katika ofisi zao Kiembesamaki, kuzungumzia namna ZFA inavyokusudia kujisafisha mbele ya umma wa Wazanzibari.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.