Na Hafsa Golo
KAMPUNI za simu za mkononi zimedaiwa zikikiuka taratibu za usajili wa laini za simu wa kutumia vitambulisho vya mteja badala yake mawakala wao wamekuwa wakibuni mbinu mbadala katika usajili huo, ili tu ‘mteja asirudi’.
Mawakala hao wamekuwa wakitoza shilingi 1,000 kwa ajili ya usajili wa laini mpya, iwe mteja ana kitambulisho halali au la.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi katika manispaa ya Zanzibar, umebaini kuwepo mawakala wa kampuni za simu ambao wamekuwa wakiuziwa wateja laini mpya na baadae kuwasajili kama taratibu zilivyo, lakini wateja wanapodaiwa vitambulisho ramsi kama Zan ID, hudai kuwa hawana kitambulisho chochote, lakini mawakala huwasajili huku wakiwataka wateja hao kuwaletea kitambulisho siku inayofuata kitu ambacho huwa hakifanyiki, huku laini hizo zisizosajiliwa kihalali zikiendelea kutumia.
Uchunguzi huo umebaini mara nyingi laini hizo hutumika kufanya uhalifu, ikiwemo kuwashambulia kwa maneno makali baadhi ya watu na kutoa lugha za vitisho.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) iliyaagiza makampuni yote ya simu kusajili laini za wateja wao na kusema itazifungia laini zote za simu ambazo hazijatumika.
Wakala Khalfan Omar ambae anasajili laini za simu za kampuni ya Zantel na kampuni ya Vodacom na Airtel, alisema hakuna ulazima wa mteja kukosa huduma hiyo kwa kuwa hana kitambulisho kwani kuna tararibu ambazo wanazitumia katika usajili huo bila ya mhusika kuwa na kitambulisho.
Naye Amina John wakala anaesajili na kuuza vocha za kampuni ya Tigo alisema anabuni jina na tarehe ya kuzaliwa pamoja na nambari ya kitambulisho katika utendaji wake wa usajili pale ambapo mteja atakuwa hana kitambulisho.
Pia alisema amekuwa akitumia vitambulisho ambavyo vimeshatumika kusajiliwa kwenye kampuni nyengine za simu.
Kwa upande wa Afisa Masoko kampuni ya Airtel Zanzibar, Simeo Magelanga, alikiri kuwepo ukiukwaji wa taratibu za usajili wa laini za simu unaofanywa na mawakala kutokana kuweka mbele maslahi yao binafsi.
Alisema hali hiyo inaifanya Airtel kukumbwa na changamoto kutokwa kwa wateja ikiwemo kufika makao makuu ya kampuni hiyo kutoa malalamiko ya kudai kutukanwa na kushambuliwa kwa maneno makali.
Aidha alisema mamlaka ya mawasiliano iwapo inabaini ubabaishaji na ukiukwaji wa taratibu uliowekwa kampuni husika hupigwa faini sambamba na kufungiwa kwa laini za wateja jambo ambalo husababisha kampuni kupoteza mapato.
"Kampuni haikubaliani na mwenendo unaofanywa na mawakala kwani ni kuzorotesha ufanisi wa kampuni na kuna baadhi ya vijana tayari tumewafungia huduma kwa kukiuka taratibu zilizowekwa hasa tukizingatia kwamba kampuni ikigundulika inakwenda kinyume na taratibu inapingwa faini," alisema.
Mkurugenzi wa biashara wa kampuni ya Zantel Zanzibar, Mohammed Khamis Mussa, alisema suala hilo limekuwa sugu kwani mawakala wamekuwa wakikiuka taratibu za usajili sambamba na kuuza laini kwa kiwango cha juu badala ya shilingi 500 na kutakiwa kusajili bure, badala ya kumtoza mteja shilingi 1,000.
Hata hivyo waliwataka wananchi wasikubali kuuziwa laini zilizokuwa zimesajiliwa kinyume na taratibu kwani inaweza kumsababishia matatizo.
Afisa wa ngazi za juu ambae hakutaja jina lake litajwe kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kudai kwamba si msemaji wa mamlaka hiyo, alisema iwapo watabaini laini ambazo zimesajiliwa kinyume na taratibu watazifungia.
No comments:
Post a Comment