Na Mwanajuma Mmanga
KIKOSI cha kudhibiti dawa za kulevya uwanja wa ndege wa Zanzibar, kinamshikilia raia mmoja wa Ugiriki baada kukutwa na shehena ya dawa za kulevya aina ya cocaine zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 200.
Mgiriki huyo alietambuliwa kwa jina la Vasileios Nitis (24) alikamatwa na dawa hizo zenye uzito wa kilogramu nne.
Dawa hizo alikuwa amezihifadhi katika begi lake la nguo.
Kwa mujibu wa taarifa za Polisi,mtuhumiwa huyo alikuwa akitokea Dar es Salaam kupitia Zanzibar akijiandaa kupanda ndege ya shirika la ndege la Kenya (KQ) kuelekea nchini Italia.
Kukamatwa kwake kunatokana na taarifa zilizotolewa na Polisi wa kimataifa (Interpol) ambao walikuwa wakifuatilia nyenendo za mtuhumiwa huyo.
Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa, amethibitisha kutiwa mbaroni Mgiriki huyo akiwa katika kituo chake cha mwisho kuondoka nchini akiwa na dawa za kulevya kabla ya kuziingiza Italia.
Kamishna Mussa alisema kiwango cha dawa za kulevya alichokuwa nacho mtuhumiwa huyo ni kikubwa kuwahi kukamatwa katika uwanja wa ndege wa Zanzibar.
Zaidi ya watu sita wamekamatwa katika uwanja huo wa ndege wa Zanzibar mwaka uliopita wakisafirisha dawa za kulevya.
Mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.
No comments:
Post a Comment