Habari za Punde

Tenga: Vijeba wasipenyezwe Copa Coca Cola


 
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
 
RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga, amewaasa viongozi wa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa kutokuingiza wachezaji waliozidi umri kwenye michuano ya U-15 FIFA Copa Coca-Cola 2013.
 
Amesema si vyema kwa viongozi hao kufanya ujanja na kutumia wachezaji vijeba, hatua aliyosema inawanyima fursa wanasoka chipukizi wenye haki ya kushiriki mashindano hayo.
 
Wito huo ameutoa jana wakati akifungua semina elekezi ya michuano ya Copa Coca-Cola ambayo kuanzia mwaka huu itakuwa ikishirikisha watoto wenye umri chini ya miaka 15.
 
  Rais Tenga amesema hakuna jambo la kipuuzi kama kuchomekea wachezaji waliozidi umri unaotakiwa kwa vile lengo la michuano ya aina hiyo ni kubaini vipaji na kuwafanya watoto wapende kucheza mpira wa miguu. “Kwanza nawashukuru kwa kutenga muda wenu na kuhudhuria semina. Lakini ni vizuri pia mkahakikisha mnakuwepo kwenye mashindano ili kutekeleza haya ambayo tutakubaliana katika semina hii. Mkileta mtu mwingine anaweza kutuanzishia mambo mengine badala ya yale tutakayokubaliana,” amesema Tenga.

  Pia ameishukuru kampuni ya Coca-Cola ambayo imekuwa ikidhamini michuano hiyo tangu mwaka 2007.
 
Semina hiyo elekezi inayoshirikisha makatibu wa vyama vya soka vya mikoa na waratibu wa mikoa wa michezo ya UMISSETA ni ya saba mfululizo.
 
Ratiba ya michuano hiyo kuanzia mwaka huu imebadilika ambapo sasa itaanzia ngazi ya wilaya mwezi Aprili wakati fainali katika ngazi ya Taifa itachezwa Septemba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.