Habari za Punde

Utalii kuwa ndoto kama suala la amani na utulivu halitazingatiwa - Balozi Seif

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Watalii kutoka Afrika ya Kusini, akiwa katika ndege hiyo baada ya kuzindua safari yake kwa Zanzibar. 

 
 Kaimu Waziri wa Habari Michezo Utamaduni na Utalii Juma Duni kulia akizungumza na Mwakilishi wa Shirika la Fly Mango Airlines Javed Jaffery na Mwenyekiti wa ZATI Abdulsamad Said,baada ya uzinduzi wa Ndege hiyo. 
 Rubani wa Ndege ya Shirika la Mango Airlines Kepteni Kevin Viljoen akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif mara baada ya kutua kwenye uwanja wa ndege wa Zanzibar kuanza safari za kuleta abiria kati ya Afrika Kuisni na Zanzibar.
Nyuma ya Kepteni Kevin ni Kaimu Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mh. Juma Dunia Haji.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akimaliza kuzindua safari za ndege za shirika la Mango Airlines kati ya Afrika Kusini na Zanzibar hapo uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar uliopo Kisauni.
Kulia yake ni Kaimu Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mh. Juma Duni Haji na Kushoto yake ni Mwakilishi wa Shirika la Mango Airlines hapa Zanzibar Bwana Javed Jaffery.
 Baadhi ya Watalii 175 waliotua uwanja wa ndege wa Zanzibar kwa kutumia ndege ya shirika la Mango Airlines wakifurahia ukarimu wa kinyaji cha dafu mara tuu bada ya kutua uwanja hapo.

Kaimu Waziri wa Habari Utamaduni na Utalii Juma Duni, akitowa maelezo wakati wa Safari za Ndege ya Watalii kutoka Afrika ya Kusini ilioaza safari zake Zanzibar.  
Viongozi wa Kamesheni ya Utalii Zanzibar wakimsikiliza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akizinduzi safari za Ndege ya Fly Mango iliowasili katika Uwanja wa Kimataifa wa Amani Abeid Karume ikiwa na Watalii 175,wakitokea Afrika ya Kusini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisoma hotuba ya uzinduzi rasmi wa safari za watalii kutoka moja kwa moja Afrtika kusini hadi Zanzibar kwa usafiri wa shirika la Mango Airlines hapo uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar Kisauni Nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR-ZNZ.

Na Othman Khamis Ame OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema asilimia 80% ya mapato ya fedha za kigeni zinazoingia Nchini kupitia Sekta ya Utalii inaweza kubakia kuwa ndoto kama suala la amani na utulivu halitazingatiwa na kupewa nafasi yake chini ya usimamizi wa Jamii kwa mashirikiano na Serikali Kuu.

Alisema hakutakuwa na mgeni wala Mtalii atakayekuwa na shauku ya kutaka kuingia Nchini sambamba na kufifia biashara ya Utalii endapo amani na utulivu uliopo utachezewa na hatimae kutoweka kabisa.

Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati akizindua rasmi safari za ndege za shirika liitwalo Mango Airlines kati ya Afrika Kusini na Zanzibar kufuatia ushawishi uliofanywa na Kampuni ya utembezaji watalii Zanzibar ya Gallery Tours, hafla iliyofanyika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar uliopo Kisauni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.



Alisema Taasisi, Jumuiya na hata watu waohudumia wageni na watalii wanapaswa kuendeleza zaidi ukarimu uliopo Nchini ambao ni miongoni mwa utamaduni unaoikuza Zanzibar Kiutalii katika Mataifa ya Nje.

“ Hakika vivutio tulivyokuwa navyo mfano Utamaduni, fukwe, bustani za ndani ya Bahari, Mambo ya kale , wanyama adimu ni mali kubwa, lakini mali zaidi katika vyote hivyo ni amani na utulivu”.Alisisitiza Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba Serikali kwa upande wake itajitahidi kutunza na kuidumisha amani na wale wanaotishia usalama wa wananchi na mali zao watachukuliwa hatua zinazostahiki kwa mujibu wa sheria bila ya kumuonea mtu.

Ameipongeza Kampuni ya Gallery Tours kwa uratibu wake uliofanikisha Kampuni ya Mango Airlines kuanzisha safari zake kati ya Afrika ya Kusini na Zanzibar na kuyataka Makampuni mengine popote pale yalipo kuanzisha safari kama hizo baina ya mataifa mbali mbali duniani na Zanzibar.

Balozi Seif ameyahakikishia makampuni yatakayotumia fursa hiyo kuwa Serikali itayapatia mashirikiano ya hali ya juu lengo likiwa ni kurahisisha uingiaji wa watalii ili kuimarisha sekta hiyo muhimu kwa sasa.

Alifahamisha kwamba safari za ndege zitakazofanywa na Kampuni ya Mango Airlines kati ya Afrika Kusini na Zanzibar ni miongoni mwa kishawishi kitakachoongeza idadi ya watalii wanaotoka Nchini humo kutembelea Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema soko hilo la Afrika Kusini ni kubwa na ni lazima kwa makampuni yanayohusika na sekta hiyo kujiimarisha ili kupata watalii wengi zaidi.

“ Mwaka 2012 watalii kutoka Afrika Kusini ni kubwa na ilifikia watalii elfu 11,145 na kuchukuwa nafasi ya Tano miongoni mwa Nchi zilizoleta watalii wengi hapa Zanzibar”. Alifafanua Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iiddi aliipongeza Wizara ya Habari, Utamaduni ,Utalii na Michezo Zanzibar kwa juhudi zake zilizopelekea kufanikisha harakati hizi za kukuza utalii nchini.

Akimkaribisha mgeni rasmi katika uzinduzi huo Kaimu Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mh. Juma Duni Haji alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini moyo na juhudi za Makampuni hayo kwa uwamuzi wao wa kuekeza katika sekta ya Utalii ambayo ni sehemu ya muhimili wa Uchumi wa Taifa.

Mh. Juma Duni alifahamisha kwamba Serikali inaelewa kwamba vipo vivutio vingi vya ushawishi wa Utalii katika Mataifa mbali mbali Duniani lakini kampuni hizo zikaonelea kufanya biashara zao hapa Zanzibar.

Kaminu Waziri huyo wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo alieleza kuwa muelekeo wa utoaji wa huduma za Utalii zitaongeza kiwango cha mchango wa fedha za kigeni kupitia Sekta hiyo.

Mapema Mwakilishi wa Kampuni ya Mango Airlines hapa Zanzibar Bwana Javed Jaffery alisema safari za ndege za Kampuni hiyo kati ya Afrika Kusini na Zanzibar zilianza Disemba mwaka uliopita lakini zikasitishwa kutokana na upungufu wa abiria kati ya pande hizo mbili.

Bwana Jaffery alieleza kwamba kuanza tena kwa safari hizo kumekuja kutokana na ongezeko la idadi ya makampuni yanayoshughulikia sekta ya Utalii kushawishi abiria kutumia kituo cha Zanzibar kama kiunganishi kwa safari zao katika Mataifa mengine Duniani.

Jumla ya abiria mia moja na Sabini na Tano wameteremka kutoka ndani ya ndege hiyo ya Mango Airlines ikitokea moja kwa moja Afrika Kusini chini ya usimamizi wa Rubani wa Ndege hiyo Kepteni Kevin Viljoen na wana anga wenzake.

1 comment:

  1. mwanzo unakuwa mzuri lakini baadae huwa mnachemsha kwa kujidhalilisha kwa kudai vipasenti viingie kwenye akaunti zenu za binafsi huko majuu , kwa hio wito wangu viongozi wahusika hebu ridhikeni na maisha yenu ya mishahara ya halali , muangalie maslahi ya wananchi na nchi ktk uwekezaji wowote ule , acheni tabia ya vipasenti halafu wengine mnaenda kuhiji au kufuturisha kumbe vipato vyenu vina kila uharamu

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.