Na Hafsa Golo, Mwashamba Juma
WIZARA ya Habari Utamaduini Utalii na Michezo, imeshauriwa kuzingatia zaidi ushauri uliochangiwa na wadau wa habari katika kuifanyia marekebisho sheria namba tano ya magazeti ya mwaka 1988 ili kwenda sambamba na wakati uliopo.
Walisema wakati umefika wa kufanyiwa marekebisho kwa sheria hiyo kutokana na kuwa haiwezi kukidhi haja kwa baadhi ya vipengele vilivyomo ambavyo vimekuwa ni changamoto kwa wahusika wa sekta hiyo.
Ushauri huo ulitolewa jana na wadau wa habari walipokuwa wakitoa mapendekezo ya marekebisho ya sheria hiyo katika ukumbi wa Bwawani mjini hapa.
Kurekebishwa kwa sheria hiyo kunatokana na ukongwe wa sheria yenyewe ambapo umeonekanwa kuegemea katika mfumo wa habari iliokidhi zaidi matakwa ya vyombo vya habari vya serikali.
Akichangia mada Khadija Khamis kutoka Idara ya Habari Maelezo alisema sheria hiyo ina mapungufu mengi na haifai tena katika mazingira ya sasa.
Naye Moza Saleh kutoka Hit FM alisema kuna baadhi ya vipengele vimekuwa vikiwapa mamlaka makubwa baadhi ya watendaji jambo ambalo linaweza kusababisha kiburi katika maamuzi bila ya kuzingatia sheria.
“Kumpa mamlaka moja kwa moja kiongozi tukumbuke yule ni binaadamu hivyo ni vyema kuzingatia zaidi sheria kwani sheria ni msumeno haichaguwi inamkumba kila mmoja anaekiuka,” alisema.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Fakih Haji Mbarouk alisema muongozo mzuri wa sheria ni ule ambao utaendana na mazingira yaliopo huku ukitatua changamoto sambamba na kuondokana na vikwazo visivyo vya lazima katika kukabiliana na utendaji wa majukumu ya kihabari.
Hata hivyo alishauri kutoifanyia haraka sheria mpya hiyo ili ipatikane sheria madhubuti ambayo itaepukana na migogoro na kurejea makosa ya nyuma ambayo hayawezi kutoa muongozo sahihi.
Mapema mshauri wa masuala ya sheria na mwandishi wa habari kutoka shirika la magazeti ya serikali, Juma Khamisi alikiri kuwepo kwa mapungufu ya sheria hiyo hivyo aliwashauri wadau hao kuwasilisha mapendekezo yao kwa upana yatakayokidhi mahitaji ya sasa na yajayo.
Alisema iwapo kutakuwa na umakini wa kutoa maoni sahihi yatakayokidhi mahitaji ya watumiaji sambamba na utumiaji wa sheria hivyo hakutokuwa na vikwazo katika marekebisho ya sheria hiyo.
No comments:
Post a Comment