Na Bashir Nkoromo,China
ZAIDI wa watu milioni 230 wamekuwa wakihama kila mwaka kutoka vijijini kwenda kutafuta kazi zilizo bora mijini nchini China, jambo ambalo limeelezwa kuwa ni moja ya changamoto kubwa zinazokwaza mikakati ya kupunguza umasikini vijijini katika nchi hiyo yenye watu zaidi ya bilioni moja.
Akitoa mada kuhusu China ilivyofanikiwa katika kupunguza umasikini vijijini, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Kituyo cha Kimataifa cha kupunguza umasikini, Profesa Huang Chengwei, alisema changamoto nyingine zinazozikabili juhudi hizo, ni watu kuishi maeneo yasiyofaa kwa kilimo kama yenye miamba mingi ya mawe, ukame na yanayokumbwa na magonjwa ya mlipuko mara kwa mara.
Proifesa Chengwei alitoa mada hiyo katika semina iliyoandaliwa na uongozi wa Chama Cha Kikomunisti cha China (CPC) kwa ajili ya ujumbe wa viongozi 14 wa CCM, ulioko katika ziara ya mafunzo nchini humo ukiongozwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, kwa mwaliko wa chama cha CPC.
Alisema, licha ya changamoto hizo, kitakwimu hali ya uchumi wa China imekuwa na kuifanya nchi hiyon kuwa ya pili duniani na kwamba ili kuhakikisha ukuaji wa kweli wa uchumi unafikiwa katika nchi hiyo, kigezo ni hali ya maisha ya watu wa vijijini ambayo alisema, kwa sasa yanakuwa bora kwa haraka kuliko mijini.
Profesa Chengwei alisema, wakati hali ya umasikini kwa wakazi wa vijijini nchini China ilikuwa asilimia 8.35 mwaka 1981, kiwango hicho cha umasikini kilishuka kadi kufikia asilimia 1.78 mwaka 2008 na kwamba hali imeendelea kuimarika kutokana na serikali kuwekeza juhudi kubwa kwenye kilimo.
Alisema, hadi sasa China inachopambana nacho ni kukuza kipato kwa kila mwananchi hasa wa vijijini, kwa kuwa sasa nchini humo hakuna umasikini katika suala la nguo na chakula kwa wananchi wake kama ilivyokuwa katika kipindi cha miaka 30 iliyopita wakati China ikiwa katika kundi la nchi zinazoendelea.
Huku akionyesha takwimu mbalimbali zinazoonyesha kupanda haraka kwa kipato kwa kigezo cha maeneo ya vijijini, Profesa Chengwei alisema, China imefanikiwa baada ya kutumia wataalam wa ndani na nje na kuibua mpango kamambe wa kuunda vikundi au taasisi za kupunguza umasikini vijijini.
Alisema, baada ya kuundwa vikundi hivyo, viliwekwa na kusimamiwa tangu ngazi ta taifa hadi vijijini na kila mmoja kubeba jukumu la kuhakikisha yanapatikana mafanikio kila alipo.
Profesa Chengwei alisema, pamoja na kushirikisha maeneo yote, juhusi hizo zilishirikisha pia mataifa na taasisi za nje za fedha, jambo ambalo alisema, lilichangangamsha mpango huo na kusababisha mafanikio ya haraka.
Pamoja na Kinana viongozi wa CCM walioshgiriki semina hiyo, ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Zanzibar) Vuai Ali Vuai, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Khadija Aboud, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Dk. Asha-Rose Migiro, Mweneyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu, Dk. Titus Kamani, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa mjini Magharibi Yusuf Mohamed Yusuf na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu.
Wengine ni Katibu Mkuu wa CCM wa Umoja wa Vijana wa CCM, Martine Shigela, Katibu Mkuu wa Jumuia ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Amina Makilagi na Katibu Mkuu wa Umoja wa Wazazi Tanzania, Khamis Suleiman Dadi na Katibu wa CCM mkoa wa Mbeya Maganga Sengelema na maofisa wa Chama, Bashir Nkoromo na Edward Mpogolo.
No comments:
Post a Comment