Habari za Punde

Walala kwenye mabanda ya kuku. • Wafanyakazi shamba la mipira wadai kunyanyaswa.

Mwantanga Ame
VIONGOZI wa Ushirika wa Watu Wenye Ulemavu unaoshughulikia ufugaji kuku Upenja,wameamua kugeuza mabanda ya kuku kuwa vyumba vya kulala baada ya mradi wao kutoenda vizuri.

Kiongozi wa ushirika huo, Juma Mtendo Haji aliyaeleza wakati Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi alipofanya ziara katika ushirika huo.

Alisema wamelazimika kulala ndani ya mabanda hayo baada ya ufugaji wa kuku kutokuwa mzuri.

Alisema hapo awali mradi huo ulifadhiliwa majengo na Mfuko wa TASAF, baada ya kupatiwa shilingi milioni nane ambapo ujenzi wa mabanda hayo ulitumia shilingi milioni 6 .4 na shilingi milioni 1.4 walinunulia vifaranga vya kuku na kuwaweka katika mabanda hayo.

Alisema baada ya kuuza kuku hao waliamua kujenga banda la pili, lakini mradi wao haukuenda vizuri na sasa wanafikiria kubadili aina nyengine ya mifugo.

Alisema mtaji walionao sasa ni shilingi 700,000 pekee ambazo hazitoshi kuendesha mradi wa ufugaji kuku.

Balozi Seif akizungumza na wanaushirika huo alisema ataangalia namna ya kuwasaidia kwani kinachokosekana ni suala la usimamizi bora wa mradi.

Wakati huo huo, wananchi wa kijiji cha Kirombero wanatarajiwa kuondokana na tatizo la muda mrefu la ukosefu wa maji baada ya kisima kilichochimbwa kikiwa katika hatua za mwisho kuanza kutoa huduma.

Kisima hicho kimejengwa kwa msaada wa Balozi Seif na kugharimu zaidi ya shilingi 20,000,000.

Balozi Seif alikabidhi vifaa vya ujenzi ikiwa ni pamoja na matofali, saruji na mchanga ili kuendeleza ujenzi wa jengo litakalokuwa hifadhi ya kisima hicho.

Akizungumza na wananchi wa kijiji hicho, Balozi Seif alielezea matumaini yake kwamba kukamilika kwa kisima hicho itakuwa ni hatua kubwa kwa wananchi hao ya kupata maji yenye uhakika.

Aliwaeleza wananchi hao kwamba tatizo la uhaba wa maji bado linaendelea kuyakabili maeneo mengi nchini mjini na hata vijijini, lakini serikali itaendelea na jitihada kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo kumaliza changamoto hizo.

Balozi Seif pia alipata fursa ya kutembelea ujenzi wa jengo jipya la skuli ya maandalizi na baadaye kuangalia msingi wa ujenzi wa skuli ya msingi Pangeni na kupongeza jitihada za wananchi wa kijiji hicho katika hatua za kuwajengea mazingira bora ya kielimu watoto wao.

Balozi Seif katita kuunga mkono juhudi za wananchi hao, aliahidi kuchangia nondo 15 na saruji mifuko 30 ili kuendeleza ujenzi huo ulioanza mwaka 2010 kwa nguvu za wananchi.

Mapema Balozi Seif alikagua nyumba ya walimu ya skuli ya Upenja na kuridhika na hatua iliyofikiwa jambo ambalo limempa faraja iliyomshawishi kuahidi kusaidia hatua za mwisho za ujenzi wa kisima cha skuli hiyo ili kiweze kutoa huduma baada ya kukamilika kwake.

Wakati huo huo wafanyakazi wa shamba la mpira wilaya ya Kaskazini ‘B’ wamemlalamikia Balozi Seif, kunyanyaswa na mmiliki wa shamba hilo kwa kudai hawatendei haki.

Mmoja wa wafanyakazi hao aliyetambulika kwa jina la Fadhil Wahab, mkaazi wa Kichungwani alisema kwa muda sasa wafanyakazi wa shamba hilo wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la kukosa haki zao za msingi na kufanya kazi katika mazingira magumu na manyanyaso.

Alisema malalamiko yao walishayafikisha katika ngazi mbali mbali za uongozi wa Mkoa, akiwemo mkuu wa mkoa wa Kaskazini lakini hakuna kitu walichoambulia.

Alisema hawafahamu wanafanya kazi katika mazingira gani kwani mkataba wa muwekezaji huyo umemalizika tokea 2003, lakini bado anaendelea kufanya kazi huku wafanyakazi wakishindwa kuwalipa wafanyakazi haki zaao.

Alisema ni vyema serikali ikaingilia kati kushughulikia suala hilo kwani, tayari wafanyakazi wa kiwanda hicho hawana imani na muwekezaji.

Aidha alisema kilio chao pia walishakifikisha katika taasisi za kusimamia kazi, lakini nako walikosa jibu la msingi kutoka kwa viongozi wa taasisi hizo.

Akilitolea ufafanuzi suala hilo, Balozi Seif alisema serikali kwa muda mrefu imekuwa ikisikia kuwepo tatizo hilo na kusema atakutana na uongozi wa shamba hilo kuzungumzia suala hilo.

Alisema atahakikisha kabla ya kikao kijacho cha Baraza la Wawakilishi anafanya tena ziara katika shamba hilo ili kuona namna ya kutatua matatizo hayo.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.