Na Khamis Haji, OMKR
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ameitaka jamii isiruhusu watu wanaojihusisha na kuuza dawa za kulevya pamoja na matendo mengine maovu, kama vile ukahaba katika maeneo yao, ili kulinda mila, maadili na silka njema za Wazanzibari.
Alisema matendo hayo yanashika kasi katika mitaa ya Zanzibar na kuharibu maadili mema kutokana na jamii ya Wazanzibari kuanza kuiacha tabia ya malezi ya watoto kwa pamoja, na sasa kila mtu kuhusika na lake.
Alieleza hayo alipokuwa akihutubia katika sherehe za Maulid ya kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W) zilizoandaliwa na Madrasatul Tahfidhil Quran ya Mombasa Zanzibar juzi usiku.
Alisema inasikitisha kuona katika mitaa mbali mbali Zanzibar, wananchi wanazijua nyumba ambazo kunauzwa dawa za kulevya na nyengine kufanywa ukahaba, lakini jamii katika maeneo hayo huachia mambo hayo yatendeke, kama vile hawayaoni.
Alieleza kuwa wananchi lazima waelewe kuwa wanapoachia tabia kama hizo ziendelee ni hatari kwa jamii nzima na hata wao wenyewe, kwa sababu hata watoto wao wanaweza kushawishiwa nao kujiingiza katika matendo hayo.
“Hali inavyoonekana sasa ni kama vile kila mtu na lake, ile tabia ya malezi ya pamoja inaanza kusahaulika, lazima tukumbuke unapomuona mtoto wa mwenzako anaingia kwenye maovu, kesho inaweza kuwa ni zamu ya mtoto wako,” alionya Maalim Seif.
Aliwahimiza wazazi kutilia mkazo suala la kuwasomesha watoto wao katika fani tafauti, iwe masomo ya skuli na kwenye madrasa, ili kuwaandaa kuwa raia wema walioelimika.
Hata hivyo, aliwataka wananchi wote kuwa macho na baadhi ya watu walioamua kupotosha hali halisi juu ya Zanzibar na kuihusisha kuwa inakabiliwa na tafauti kubwa za udini.
Alisema kwa dahari Zanzibar imekuwa na uvumilivu mkubwa wa kidini na watu wake wamekuwa wakiabudu kwa uhuru mkubwa bila ya kubughudhiwa, licha ya kuwa asilimia 98 ya wananchi wa Zanzibar ni waislamu.
Wana madrasa hao katika risala yao kwa Makamu wa Kwanza wa Rais aliwahimiza viongozi na wananchi wenye uwezo kusaidia harakati za kuendeleza madrasa nchini, ikiwemo kuwasaidia walimu wa madrasa hizo ambao wengi wao wanakabiliwa na hali duni za kimaisha.
No comments:
Post a Comment