Habari za Punde

Wazazi wahimizwa kushirikiana malezi ya watoto

Na Abdi Suleiman,Pemba
WAZAZI kisiwani Pemba, wametakiwa kurudisha maelezi ya pamoja katika kuwalea watoto wao ili kuweza kupunguza vitendo vya udhalilishaji wa wanawake na watoto.

Wito huo umetolewa na Mwakilishi kutoka, Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar, tawi la Pemba, Salum Abdalla, katika ukumbi wa michezo Gombani, wakati akichangia mada, katika kongamano la kuadhimisha siku ya wanawake Duniani.

Alisema mashirikiano ya pamoja katika malezi ya watoto ndio kitu muhimu peke kitakachoweza kupunguza vitendo vya udhalilishaji na unyanyasaji wa wanawake na watoto.

Naye Raya Ali Othmani, mwanafunzi kutoka skuli ya sekondari Tumbe, aliwataka wazazi kuwapunguzia kazi watoto, ili wapate muda wa kupumzika na kupitia mabuku yao.

Alisema wazazi wamekuwa wakiwapa kazi nyingi watoto hasa wa kike, hali inayowafanya kufeli katika mitihani yao ya darasani na kitaifa.

Zuwena Hamad Ali, kutoka dawati la polisi wanawake, aliiomba serekali kuhakikisha inafanya kila linalowezekana kununua mashine ya DNA ili kupunguza malalamiko ya wananchi.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya wanawake na watoto, Rabia Rashid Omar, alisema chimbuko la siku hiyo ni kuwakumbuka wanawake wenzao waliokuwa wakifanyishwa kazi ngumu katika viwanda mnamo miaka ya 1886 nchini Marekani.

Kwa upande wake Afisa Mdhamini wa Wizara ya Ustawi wa Jamii Maendelo ya Wanawake na Watoto Pemba, Maua Makame Rajab, alisema kuwepo kwa wizara ya wanawake na watoto ni moja ya hatua kubwa iliyochukuliwa na serikali katika kuwaondolea wanawake matatizo yaliyokuwa yakiwakabili.

Hata hivyo, aliwataka wananchi wa kisiwa cha pemba kuendela kukitumia kituo cha mkono kwa mkono kilichomo hospitali ya Chake Chake, kwa kuripoti kesi za udhalilishaji wa wanawake na watoto.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.