Na Ameir Khalid
CHAMA cha Soka Zanzibar (ZFA) Wilaya ya Mjini, kimezitaka taasisi za serikali na binafsizinazokusudia kuleta wageni kwa ajili ya sherehe za pasaka mwaka huu, kuhakikisha zinapeleka taarifa na majina ya wageni wanaokusudia kuwaalika katika ofisi zake zilizopo Amani.
Katibu wa ZFA wilayani humo Yahya Juma Ali, amesema kuwa kisheria chama chake ndicho chenye dhamana ya kuratibu ujio wa vikundi na wageni wote wanaohudhuria sherehe hizo kila mwaka.
Aidha, amevitaka vikundivyote vinavyotarajia kupokea wageni hao, kufika katika ukumbi wa VIP uwanja wa Amani Machi 24, kwa ajili ya kupanga mipango ya kufanikisha sherehe hizo.
Alisema kuwa, endapo vikundi vitashindwa kuwasilisha majina ya wageni wao, ZFA haitakuwa na dhamana ikiwa kutajitokeza matatizo ya aina yoyote.
Alifahamisha kuwa, ni vikundi vitano tu kati ya 50 vinavyotarajiwa kushiriki tamasha hilo,ambavyo vimeweza kuwasilisha majina ya wageni wao.
Amevitaja vikundi hivyo kuwa ni timu ya soka ya Mafunzo, tawi la CCM Shaurimoyo, tawi la Karakana, Chumbuni na ZFA Wilaya ya Magharibi.
Sherehe za pasaka ambazo hufanyika kati ya wiki ya mwisho ya mwezi Machi na ya kwanza Aprili kila mwaka, kwa wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar kutembeleana kwa zamu, mwaka huu zinafanyika Zanzibar kuanzia Machi 29 hadi Aprili 4, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment